Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil, Carlos Dunga amemuongeza kiungo wa klabu ya Orlando City ya nchini Marekani, Ricardo Kaka, kwenye kikosi chake ambacho kipo katika maandalizi ya mwisho ya fainali za mataifa ya kusini mwa Amerika (Copa America).

Dunga amemuita kiungo huyo mwenye umri wa miaka 34, baada ya kumuondoa kiungo wa mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, Douglas Costa, ambaye anasumbuliwa na majeraha ya paja la mguu wake wa kushoto.

Douglas Costa

Kaka ameongezwa katika kikosi cha Brazil na kuwa na matumaini ya kuichezea tena timu ya taifa ya nchi yake, ambapo kwa mara ya mwisho alifanya hivyo mwaka 2012.

Kiungo huyo ambaye aliwahi kuzitumikia klabu nguli barani Ulaya AC Milan na Real Madrid, amekuwa mchezaji wa pili kuitwa kikosini kwa lengo la kujazia nafasi, akitanguliwa na mshambuliaji wa klabu ya Benfica, Jonas Gonçalves Oliveira aliyechukua nafasi ya Ricardo Oliveira.

Timu ya taifa ya Brazil, imepangwa katika kundi la pili (B) katika fainali za Copa America sambamba na Ecuador, Haiti na Peru.

Mwishoni mwa juma hili (Siku ya jumapili) Brazil itacheza mchezo wa mwisho wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Panama katika mji wa Denver nchini Marekani, kabla ya kuanza kwa fainali za Copa America Juni 04.

 

Adalipa yawafikia wanafunzi vyuoni.
Mapendekezo Ya Jackson Mayanja Yaiweka Simba Njia Panda