Chama cha soka nchini England (FA) kimeendelea kumkalia kooni meneja wa Manchester United Jose Mourinho, kufuatia tuhuma za kutoa lugha inayodhaniwa haifai michezoni, wakati wa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Newcastle United uliochezwa Oktoba 06, kwenye uwanja wa Old Trafford.

FA walimfungulia mashataka meneja huyo kutoka nchini Ureno siku moja baada ya mchezo huo, uliomalizika kwa Man Utd kupata ushindi wa mabao matatu kwa mawili.

Mourinho anadaiwa kutoa maneno machafu baada ya kikosi chake kupata bao la ushindi lililofungwa na mshambuliaji kutoka nchini Chile, Alexis Sanchez.

Hata hivyo FA wameongeza muda kwa Jose Mourinho kuwasilisha utetezi wake wa kueleza kwa kina nini maana ya maneno aliyoyatoa mbele ya kamera baada ya kufungwa kwa bao la ushindi, na kwa nini alifanya hivyo.

Mourinho amepewa hadi jumatano ya juma lijalo awe amefanya hivyo, na baadae hukumu dhidi yake itatolewa.

Endapo meneja huyo wa Man Utd atakutwa na hatia, huenda akafungiwa kukaa kwenye benchi la ufundi la Mashetani Wekundu kwa michezo kadhaa.

Kama itakumbukwa vyema katika mchezo dhidi ya Newcastle United, kikosi cha Man Utd kilikwenda mapumziko kikiwa nyuma kwa mabao mawili kwa sifuri, na kiliporejea kipindi cha pili kilifanikiwa kusawazisha kupitia kwa Juan Matta na Anton Martial kabla ya Sanchez kufunga bao la ushindi.

Rais George Weah atangaza elimu bure vyuo vikuu
Mtemi Ramadhani ajiondoa kugombea Uenyekiti Simba