Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Fiston Kalala Mayele, ametangaza dhamira ya kuendelea kufunga ‘Hat Trick’ kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.

Mshambuliaji huyo kutoka DR Congo, alifunga ‘Hat Trick’ katika michezo ya nyumbani na ugenini iliyochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, dhidi ya Mabingwa wa Sudan Kusini Zalana FC.

Mayele amesema mipango yake mikubwa ni kutaka kuendelea kufunga kwa mfumo huo kwenye michuano hiyo mikubwa Barani Afrika ngazi ya vilabu, lakini hamaanishi kama atafanya hivyo kwenye mchezo ujao dhidi ya Al Hilal ya Sudan, japo anaamini inaweza kutokea.

Amesema kufunga ‘Hat Trick’ ni bahati inayokuja kwa nadra sana, lakini ana uhakika endapo Young Africans itafanikiwa kufuzu hatua ya Makundi, atafanya hivyo katika michezo ya hatua hiyo.

“Ngumu kupanga kufunga ‘Hat Trick’ na kufanikiwa, lakini kwangu nimeweka mipango yangu msimu huu nikicheza michuano hii ya Kimataifa.”

“Nimeanza vizuri kwa kupiga ‘Hat Trick’ mbili dhidi ya Zalan FC, malengo yangu ni kuona naendelea na kasi yangu hii, kwangu naona ni mwanzo mzuri kutokana na kuongeza hali ya kujiamini ninapofikia katika goli la wapinzani wetu,” amesema Mayele

Young Africans itacheza na Al Hilal kati ya Oktoba 7-9, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, na itamalizia ugenini mjini Omdurman-Sudan kwa kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili kati ya Oktoba 14-16.

Ikiwa Young Africans itaitoa Al Hilal na kufuzu hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, itajihakikishia kitita cha fedha kiasi cha Dola za Marekani 550,000 sawa na Shilingi za Tanzania Bilioni 1.3 kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Na kama itatokea Young Africans inatolewa katika hatua hiyo, itaangukia hatua ya Mtoano Kombe la Shirikisho Barani Afrika, endapo itafuzu hatua ya Makundi itajihakikishia Dola za Marekani 275,000 sawa na Shilingi za Tanzania Milioni 641 kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Ruto ataka sentensi mpya mapambano Uviko-19
Wanne wasimamishwa kazi kupisha uchunguzi mil. 300