Kocha wa Al-Ittihad ya Libya, Diego Garzitto amedai mashindano ya klabu yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, yamegubikwa na vitendo viovu vya rushwa kwa waamuzi, ambavyo ndivyo vinaamua timu za kutwaa ubingwa na sio ubora na uwezo wa uwanjani.

Kocha huyo ameenda mbali zaidi kwa kuitaja timu ya TP Mazembe kama kinara wa kutoa rushwa kwa waamuzi ili waibebe jambo ambalo linaondoa maana halisi ya ushindani.

Akinukuliwa na mtandao wa www.mysoccer24.com mara baada ya mahojiano yake na kituo cha luninga cha Al Wasat cha Libya, Garzitto alisema kuwa nchi nyingi Afrika, viongozi wa klabu wamekuwa wakitumia nguvu kubwa nje ya uwanja hasa kuwahonga marefa na wale wanaowapa kiasi kikubwa cha fedha ndio hufanikiwa.

“Bila shaka kuna uongozi ambao unajua kushughulika na mashindano ya klabu ya Caf kwa mfano TP Mazembe wako karibu sana na marefa. Namaanisha kushindana ni lazima uwe angalau na marefa wawili au watatu katika mfuko wako,” alisema Garzitto.

Garzitto ana uzoefu mkubwa wa soka la Afrika kutokana na kuwahi kufundisha idadi kubwa ya timu ikiwemo TP Mazembe ambayo mwaka 2009 aliiongoza kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mbali na TP Mazembe na Al Ittihad, timu nyingine za Afrika ambazo Garzitto amewahi kuzifundisha ni Wydad Casablanca, Al Hila Omdurman, CS Constantine, Al Merrikh, timu ya Taifa ya Togo na timu ya taifa ya Ethiopia.

Zaidi ya watu Bilioni 3 wafuatilia tukio la kuagwa kwa Magufuli
Simba SC: Tutampa zawadi Magufuli