Mshambuliaji kutoka nchini Argentina Gonzalo Higuain anatarajiwa kukamilisha taratibu za kujiunga na klabu ya AC Milan, baadae hii leo akitokea kwa mabingwa wa soka Italia Juventus FC.

Mshambuliaji huyo jana Jumatano aliwasili mjini Milan kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya na taratibu nyingine za uhamisho wake, kabla ya kutangazwa rasmi mbele ya waandishi wa habari leo Alkhamis.

Baadhi ya mashabiki walikusanyika nje ya hoteli ya Milan (Milan Hotel) baada ya kusikia mshambuliaji huyo amefikia mjini humo, kwa shauku ya kutaka kumuona na kujiridhisha kama kweli atakua sehemu ya kikosi cha AC Milan msimu ujao.

Higuain alijiunga na mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC mwaka 2016 kwa ada ya Euro milioni 90 sawa na dola za kimarekani milioni 105 akitokea SSC Napoli, na msimu uliopita aliifungia klabu hiyo ya mjini Turin mabao 36 katika michezo ya ligi kuu (Serie A).

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30, anaondoka Juventus huku  akiacha kumbukumbu ya kutwaa ubingwa wa ligi (Serie A) na kombe la Italia (Coppa Italia) katika misimu miwili mfululizo aliyocheza klabuni hapo.

Kwa ujumla amefunga mabao 55 katika michezo 105 aliyocheza tangu alipojiunga na Juventus.

Uhamisho wa Higuain unatajwa kuhusishwa na makubaliano ya beki wa kati AC Milan Leonardo Bonucci, kurejea Juventus kama sehemu ya maazimio yaliyofikiwa na viongozi wa pande hizo mbili.

Beki huyo anapewa nafasi kubwa ya kurejea Juventus aliyoitumikia kwa miaka saba kabla ya kuondoka mwishoni mwa msimu wa 2016/17 huku akiisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi ya Italia (Serie A) mara sita mfululizo. Alijiunga na AC Milan kwa ada ya Euro milioni 40.

Jean-Pierre Bemba kuwania Urais DRC
Video: Magufuli ashusha nyundo kwa vigogo, Makonda achapwa

Comments

comments