Mshambuliaji kinda wa klabu ya Simba Haji Ugando, huenda akaondoka Msimbazi mwishoni mwa msimu huu, baada ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.

Ugando ameshindwa kujihakikishia nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza tangu alipowasili kocha kutoka nchini Cameroon Joseph Omog.

Kocha msaidizi wa Simba Jackson Mayanja aliwahi kumtumia mshambuliaji huyo wakati akikaimu nafasi ya ukuu wa benchi la ufundi msimu uliopita, na alionyesha uwezo mkubwa wa kucheza na kufunga mabao.

Kufuatia hali hiyo, meneja wa mchezaji huu Jamal Kisongo amesema, ipo haja kwa Ugando akaondoka Msimbazi ili kukinusuru kipaji chache ambacho kinatakiwa kuendelezwa kwa kucheza mara kwa mara.

Kisongo amezungumza na Dar24 na kueleza kuwa, atafanya mazungumzo na rais wa klabu ya Simba Evance Aveva, ili kupata muafaka wa kumuhamisha Ugando ambaye ana ndoto za kucheza nje ya nchi.

“Haikua makubaliano kati ya Simba na Haji Ugando ya kukaa benchi kama ilivyo sasa, kuna sehemu ya makubaliano imekiukwa, na kwa kumaliza utata huu hakuna njia mbadala ya kumnusuru zaidi ya kumtafutia mahala pengine ili acheze soka lake,” Amesema Kisongo.

“Ugando anahitaji kucheza ili aonekane, na ikiwezekana apate nafasi ya kutimiza ndoto zake za kucheza soka katika klabu kubwa nje ya Tanzania.”

Hata hivyo Kisongo hakueleza kama Ugando ataondoka Msimbazi kwa makubaliano ya kujiunga na klabu nyingine kwa mkopo ama la, lakini cha msingi ni kusubiri matokeo ya mazungumzo anayotarajia kuyafanya na rais wa klabu ya Simba Evance Aveva.

Video: Airtel yazindua duka la huduma kwa wateja Manyara
Video: Majaliwa ataka watanzania kuwa kitu kimoja