Baada ya kuikandamiza Man Utd mabao matatu kwa sifuri kwenye uwanja wake wa nyumbani usiku wa kuamkia leo, mshambuliaji Harry Kane ametamba kwa kusema, ushindi huo ni salamu tosha kwa wapinzani wa Tottenham Hotspur msimu huu wa 2018/19.

Kane ambaye alianza kupachika bao la kwanza kabla ya Lucas Moura hajafunga mabao mengine mawili ya ushindi katika mchezo huo, amesema wameonyesha kiwango kizuri tangu walipoanza msimu huu, na hatua ya kuibanjua Man Utd inaendelea kuwapa morari ya kupambana katika michezo inayokuja.

Amesema msimu huu wamejipanga kufikia lengo la kutwaa ubingwa baada ya kushindwa kufanya hivyo misimu mitatu iliyopita, tena kwa kukaribia alama za bingwa, hivyo ni jukumu lao kwa sasa, kuhakikisha jambo hilo halijirudii tena.

“Ni ushindi mkubwa kwetu, unatuweka katika mazingira ya kujiamini na kutambua ni vipi tulivyo na timu nzuri, ambayo ina uwezo wa kupambana na yoyote msimu huu wa ligi,” Alisema Kane kupitia tovuti ya klabu ya Tottenham.

“Tunahitaji kuzifunga timu nyingine katika ligi, ili kufikia lengo la kumaliza katika nafasi ya kwanza itakapofika mwishoni mwa msimu huu, ushindi wetu wa leo unatoa salamu kwa wapinzani wengine ambao tutakutana nao mbele ya safari.”

“Tulijipanga kuja hapa (Old Trafford) kushinda baada ya kujiandaa kwa kila hali, na tumefanikiwa kupata ushindi ambao nina uhakika utakua chachu ya kuendelea kufanya maajabu msimu huu.”

Ushindi wa Tottenham dhidi ya Man Utd kwenye uwanja wa Old Trafford ni wa kwanza tangu 2014.

Mwishoni mwa juma hili Tottenham watapambana na Watford, ambao pia wamefanikiwa kushinda michezo mitatu ya mwanzo ya msimu mpya wa ligi kuu ya England.

Washikiliwa na Polisi kwa kukutwa na Bangi
Ommy Dimpoz: 'Nilitia saini kufa au kupona'