Serikali kupitia Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Faustine Ndugulile imesisitiza vituo vya Afya vya Serikali kutoa huduma kwa wanawake wajawazito, watoto chini ya miaka 5 na wazee wasio na uwezo wapate matibabu bure kulingana na sera ya afya inavyosema.

Ndugulile amesema hayo wakati alipofanya ziara katika Hospitali za Rufaa Temeke, Amana na Mwananyamala jijini Dar es Salaam kujua hali ya utoaji huduma za afya.

Alisisitiza pia kila mtoa huduma anapaswa kuandika taarifa ya mgonjwa kabla na baada ya kumpa huduma katika kituo chake cha kazi.

Vilevile, amewataka watoa dawa katika hospitali na vituo vya afya kuandika majina asilia ya dawa na siyo yale ya kampuni na wafuate mwongozo wa dawa uliowekwa na serikali.

“Marufuku watoa dawa kuwaandikia wagonjwa dawa na kwenda kununua nje ya kituo cha afya, badala yake dawa zote zitolewe katika hospitali au kituo cha afya na kama zimeisha zinatakiwa kuagizwa kwa haraka na uongozi,” alisema na kuamuru kwamba wagonjwa wa wodi ya watoto waliokwenda kununua dawa nje warudishiwe fedha zao.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Temeke, Dkt. Amaan Malima, wamesema changamoto kubwa inayowakumba ni upungufu wa watumishi.

Wakati huohuo, Mkurugenzi Msaidizi wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Dkt. Meshack Shimwela, aliomba radhi kwa tatizo ambapo wagonjwa walikwenda kujinunulia dawa katika maduka ya nje, akisema hakuna tabia kama hiyo hospitalini hapo na ameahidi kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo jambo hilo.

Kwandikwa aipa tano Tanrods Manyara
Kairuki awatangazia kiama watoroshaji wa Tanzanite

Comments

comments