Mwimbaji Ray C ameanzisha vita nzito ya maneno kati yake na Hamisa Mobeto, vita iliyoanza jana kwa jiwe gizani kabla ya kujitoa hadharani baada ya kushambuliwa vikali na jeshi la ‘Team Mobeto’.

Jana, Ray C alijikuta akioga matusi ya wafuasi wa Hamisa kwenye mtandao wa Instagram baada ya kuweka picha ya nguo zenye jina kubwa la biashara la ‘Fendi’, ambazo ni aina ya nguo zinazotengenezwa na jumba maarufu la mitindo lililoko Roma nchini Italia, na kumwagika kuwa zinazodaiwa kuuzwa Tanzania ni batili au midosho.

Mwimbaji huyo alieleza mengi kwenye post zake mbili ambazo alizifuta muda mfupi baadaye, akiwatahadharisha wapenda mitindo ya nguo nchini kuwa wawe waangalifu kwani badala ya ‘Fendi’ watavalishwa ‘Feni’ na wasipoangalia watavaa na mavazi ya ‘FFU’.

Hamisa hutangaza na kuvaa nguo zenye lebo ya ‘Fendi’ ambazo anaziuza kwenye duka lake na hupost picha hizo kwenye mitandao ya kijamii. Baadhi ya nguo anazovaa Hamisa zilionekana pia kwenye post ya Ray C.

Baada ya kuzidiwa na jeshi la Team Hamisa, leo Ray C amehamia Snapchat ambapo ameweka hadharani hasira zake na kuonesha wazi kuwa anayemzungumzia ni Hamisa, huku akimponda na kumuita ‘rafiki sumu’.

‘Kiuno Bila Mfupa’ alifanya marejeo ya matukio kadhaa aliyoyafanya Hamisa dhidi ya Zari the Boss Lady ambaye pia ni mama mtoto wa Diamond.

“Umemuumiza mwanamke mwenzio waziwazi, dunia nzima inajua. Sasa mimi na wewe nani ana roho mbaya? nani mwenye wivu hapo. Nani ataanza kwenda Jehanam? Mnipishe na mateam yenu.. mxciuuu!,” Aliandika Ray C kwenye Snapchat.

Maandishi hayo pia yalionekana kuwa jibu kwa Hamisa ambaye awali alimjibu mtu mmoja kwenye Instagram akieleza kuwa anayemlalamikia kwa kutofanya biashara mtandaoni anamuonea wivu. Alihoji “ulitaka biashara mtandaoni ikufuate mpaka nyumbani?”

Kwenye majibu hayo Hamisa alionekana kuumizwa na jinsi alivyosemwa vibaya akidai kuwa watu wengine ni hadi ufe ndio wataanza kukusifia hata wakiwa maadui zako.

Aidha, kwenye ujumbe huo mrefu wa Snapchat, Ray C aliendelea kumvaa Hamisa akirejea kilichotokea kati yake na Zari.

“Umemtoa waziwazi mwanamke mwenzio kwenye nyumba! Bado kwenye 40 ukamtuza. Rafiki kama wewe ni sumu! Unalalama kuharibiwa biashara lakini wewe ndiye wa kwanza kuvunja nyumba za watu. Tell your people to stop sh*t me (waambie watu wako waache kunitusi). Nina mdomo mchafu halafu nunda!,” inasomeka sehemu ya ujumbe huo.

Haijafahamika bifu kati ya wawili hawa ilianzia wapi hadi kufikia kwenye Instagram, lakini mengi kwa watu maarufu huanzia nyuma ya kamera na nyuma ya mitandao, kinachokuja kuonekana huwa ni matokeo ya kilichoanzia walipoanzia.

Ray C kufuta post zake Instagram kumeonesha kuwa jeshi la Hamisa linaweza kukuharibia wiki, lakini bado ana sehemu nyingine ya kusemea ambapo jeshi hilo linaweza kuwa na mishale michache ya kumfikia.

Gari la wagonjwa lanaswa likisafirisha mirungi kwa ving’ora
Sheria ya kodi kwa watumiaji wa WhatsApp, Facebook kupitiwa

Comments

comments