Mabingwa wa soka duniani timu ya taifa ya Ujerumani leo watakua na kibarua kizito cha kuzuia kulipiziwa kisasi dhidi ya kikosi cha Brazil katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki.

Brazil wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa hatua ya nusu fainali ya kombe la dunia mwaka 2014, kwa kufungwa mabao saba kwa moja katika radhi ya nyumbani kwao.

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Low, amekiri kutarajia mchezo wenye ushindani dhidi ya Brazil, lakini akasisitiza bado kikosi chake kina uwezo mkubwa wa kuendeleza rekodi ya kufanya vyema.

Low ambaye alikishuhudia kikosi chake kikilazimisha matokeo ya sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Hispania mwishoni mwa juma lililopita, ameongeza kuwa, anawaheshimu Brazil kama mabingwa wa kihistoria duniani na wana nafasi kubwa ya kuendelea kudhihirisha hilo.

“Brazil wameimarika kwa kiasi kikubwa, na watakuja wakiwa na lengo la kutaka kulipiza kisasi dhidi yetu, lakini jambo hilo tumeshalitambua mapema, hivyo tutacheza kwa tahadhari kubwa huku malengo ya ushindi tukiyapa kipaumbele.”

“Tumejiandaa vya kutosha kwa ajili ya kupambana nao, tunafahamu mchezo utakua mgumu, lakini jibu litapatikana ndani ya dakika 90, tunapaswa kuwaheshimu wapinznai wetu kama ilivyo kwa timu nyingine ambazo tumeshacheza nazo.” Amesema Low.

Brazil, ambao wamepoteza mchezo mmoja kati ya michezo kumi na saba (17) waliocheza tangu walipokua chini ya kocha Tite, watamkosa nahodha na mshambuliaji wao mahiri Neymar ambaye anaendelea kuuguza majeraha ya mguu.

Kwa upande wa Ujerumani watamkosa kiungo wa klabu ya Arsenal Mesut Ozil, mshambuliaji Thomas Mueller na mlinda mlango Manuel Neuer.

Kiungo Emre Can naye ataukosa mchezo huo kufuatia majeraha ya mgongo, huku Sami Khedira akiwa katika hatihati ya kucheza baada ya kupata majeraha kwenye mchezo dhidi ya Hispania juma lililopita.

Mlinda mlango wa FC Barcelona Marc Andre ter Stegen, anatarajia kuanza langoni mwa Ujerumani akichukua nafasi ya Neuer ambaye bado majeruhu.

Katika fainali za kombe la dunia za 2018, Ujerumani wamepangwa katika kundi F sambamba na Mexico, Korea Kusini na Sweden.

Brazil wamepangwa katika kundi E sambamba na Uswiz, Serbia na Costa Rica.

Magufuli atumbua wengine wawili
Ronaldo apendekeza mbadala wa Gareth Bale.

Comments

comments