KAMPUNI inayoongoza kwa huduma mtandaoni Barani Afrika ya Mdundo, imezindua shindano la Ma-DJ, lenye lengo la kutoa fursa kwa Ma-DJ nchini Tanzania kuonyesha umahiri na vipaji vyao.

Shindano hilo, mbali na kutoa mwanya kwa Ma-DJ kuonyesha umahiri wao pia litakuwa ni fursa kwa wananchi mbalimbali kupata uelewa kuhusiana na kampuni ya Mdundo ambayo inafanya kazi na wasanii wenye vipaji wakiwemo wanamuziki zaidi ya 100,000 Barani Afrika.

Meneja Masoko wa kampuni ya Mdundo, Bw. William Abagi alisema kampeni hiyo ya mwezi mmoja, itawahusisha ma-DJ wa aina zote ambao alisema watatakiwa kuwasilisha na kuweka kazi zao (mixtapes) kwenye mtandao wa Mdundo kabla ya Desemba 10, 2021.

Alisema Tanzania iliongoza kwa idadi ya watumiaji wa miziki ya Mdundo huku ikiwa na watumiaji zaidi ya milioni 4.1 katika robo ya mwaka hadi kufikia Septemba mwaka huu huku akibainisha kuwa hii ni fursa nzuri kwa maDJ kutumia nafasi hii kujisajili ili watangaze kazi zao na kuongeza idadi ya mashabiki.

Kwa mujibu wa Bw. Abagi, DJ atakaeshinda atapata udhamini wenye thamani ya shilingi milioni saba (7,000,000/=), nusu saa ya kuonyesha umahiri wake kwenye tukio moja wapo kubwa katika moja wapo ya hafla kubwa mwakani, pamoja na muda kwenye redio.

Mshindi wa wa kampeni hiyo anatarajiwa kutangazwa Desemba 22, 2021.

“Tumeshirikiana na kampuni ya Vodacom Tanzania kuwapa wapenzi wa muziki fursa ya kupata maudhui ya muziki wa hali ya juu kutoka kwa Ma-DJ mahiri kwa bei ya chini ya hadi Tsh 100”, alisema.

Abagi alisisitiza kwamba washiriki walio na nia wanapaswa kufuata maelekezo kupitia mitandao ya kijamii ya Mdundo kwa maelezo zaidi, ambayo alisema ni pamoja na; Instagram: @mdundomusicTz, facebook: @mdundomusic, Twitter: @Mdundotanzania.

Kampuni ya Mdundo inajivunia watumiaji zaidi ya 10,500,000 kwa mwezi, walioko katika Mataifa ya Tanzania, Kenya, Nigeria, Ghana na mataifa mengine yaliyoko Barani Afrika, ambapo inafanya kazi na zaidi ya wanamuziki 100,000 wenye asili ya Afrika.

Bodi ya ATCL yaonywa
Mkurugenzi wa Gereza afungwa miaka 5 jela