Beki kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe, anaendelea vema na matibabu nchini Afrika Kusini huku ikielezwa kuwa afya yake inazidi kuimarika kadiri siku zinavyosogea.

Kapombe yupo jijini Johannesburg nchini humo katika Hospitali ya Morningside Mediclinic tokea Alhamisi iliyopita akipatiwa matibabu baada ya kugundulika na ugonjwa wa Pulmonary Embolism (donge la damu kuziba mishipa ya damu katika mapafu).

Daktari wa timu ya Azam FC, Dr. Juma Mwimbe, alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa alizopata leo kutoka huku ni kuzidi kuimarika kwa afya ya beki huyo.

“Tunamshukuru Mwenyenzi Mungu anaendelea vizuri sana, nimeongea naye leo asubuhi na ameniambia anajisikia vizuri sana na maumivu kwenye kifua yamepungua na kubakia kwa umbali sana, mpaka sasa hatujajua atarejea lini nchini kwani bado anaendelea na matibabu,” alisema.

Mwimbe alisema Kapombe anahitaji mapumziko ya miezi miwili hadi mitatu ili kuweza kurejea katika hali yake ya kawaida, hivyo atazikosa mechi zote zilizobakia za Azam FC msimu huu na huenda akarejea uwanjani kwenye kipindi cha maandalizi ya msimu ujao.

Beki huyo wa zamani wa Simba na AS Cannes ya Ufaransa, amekuwa na kiwango kizuri msimu huu kwani mpaka sasa ameshaifungia Azam FC mabao 11, nane kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), mawili Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na moja amefunga ndani ya Kombe la Shirikisho Afrika (CC) wakati timu hiyo ikiilaza Bidvest Wits mabao 3-0.

Nusu Fainali Ya Kombe La Shirikisho Hadharani
Julio Aisikitikia Simba Iliyoshindwa Kuifunga Coastal Union