Beki wa kati wa klabu bingwa Tanzania bara (Young Africans), Kevin Yondani ameshindwa kuripoti kwenye kambi ya timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa muda muafaka.

Afisa habari wa TFF Alfred Lucas amesema mpaka leo mchana beki huyo alikua hajatoa taarifa yoyote ya kutofika kambini na kuzua mkanganyiko wa sababu zilopelekea kuenguliwa katika kikosi kitakachoelekea nchini Nigeria kesho alfajiri.

“Yondani hatokuwa sehemu ya kikosi cha wachezaji kitakachoondoka kesho alfajiri kueleka Nigeria, na mpaka sasa hakuna kiongozi yoyote wa TFF mwenye taarifa rasmi, licha ya kufahamika anakabiliwa na matatizo ya kifamilia” Amesema Alfred Lucas alipozungumza na Dar24.com

Kukosekana kwa Yondani kunamuacha kocha Mkuu wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa akibakia na walinzi wa kati wawili, David Mwantika na Vincent Andrew.

Taifa Stars imepiga kambi katika hoteli ya Urban kujiandaa na mchezo wa kukamilisha ratiba ya kuwania tiketi ya kucheza  Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Nigeria siku ya Jumamosi.

Msafara wa kikosi hicho utaondoka nchini kuelekea Nigeria kesho alfajiri huku nahodha Mbwana Samatta akiwa tayari njiani kuelekea Abuja kabla ya kwenda katika jimbo la Oyo utakapopigwa mchezo huo.

Mipango Ya Pep Guardiola Yamkataa Samir Nasri
KRC Genk Yamuachia Mbwana Samatta Kwa Masharti