Faisary Ahmed – Bukoba.

Ibada ya mazishi ya mke wa mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Omkituri iliyopo kata Kibeta Manispaa ya Bukoba, imefanyika huku utata ukigubika kifo cha marehemu huyo Conchester Kabantega anayedaiwa kuuawa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Juni 13, 2023.

Mama huyo aliyekutwa amefariki huku akiwa na jeraha la kitu chenye ncha kali shingoni, amefanyiwa ibada nyumbani kwao mtaa wa Kangilwa kata ya Kibeta Mkoani Kagera, huku mumewe akiwa kituo cha polisi kwa ajili ya uchunguzi.

Akiongea katika Ibada hiyo, Mkuu wa wilaya ya Bukoba ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, Erasto Sima amesema siku ya tukio akiwa ameongozana na maafisa wa Polisi alikuta mwili wa marehemu ukiwa nje huku Mwenyekiti na mama mkwe wa marehemu wakiwa ndani wanafanya usafi.

Amesema “nikamkuta mume wa marehemu anafanya usafi wa nyumba nikachungulia kitanda kimetandikwa vizuri, katika hali ya kawaida mtu umefiwa mke wako yuko pale chini amelala wewe unadeki nyumba? Polisi inaendelea kufanya kazi yake na ndio maana mume wa marehemu hatupo nae hapa.”

Akiongoza ibada ya mazishi, Paroko Msaidizi Parokia ya Rwamishenye, Maximilian Mutasingwa amekemea kitendo hicho na kuwataka wananchi kutokufanya maamuzi wakiwa na hasira na kutaka matukio kama hayo yasitokee tena.

Awali ilidaiwa kuwa, siku ya tukio hilo mama mkwe wa marehemu, Anajoyce Deus akiwa nyumbani kwake majira ya saa 12asubuhi Juni 13, 2023 alisikia mlio wa pikipiki kwa nje na baadae watu walibisha hodi katika nyumba ya mtoto wake ambaye ni mume wa marehemu.

Alisema, “asubuhi nilikuwa najiandaa ili niende kazini lakini baadae kabla sijaamka kitandani nikasikia mlio wa pikipiki baadae nikaona imekuja moja kwa moja kwa mwenyekiti baadae wakakaa wakaongea huyo mama na kijana wa bodaboda,” alisema.

“Baada ya dakika mbili wakagonga mlango na Mimi nikawa nishaamka nakuja huku baadae nikachungulia kwenye tundu la jiko kuangalia kule kwa mwanangu kuna nini, baadae nikaona mwanangu anaenda na mimi nikamfata kwa nyuma, nikasikia mwanangu analia nikakimbia kufika pale mwanangu akasema mama huyu ameshakufa,” alisema mama huyo.

Matumla: Dulla Mbabe atamchakaza Katompa
Kampuni za Umma kufanyiwa tathmini