Kocha Mkuu wa Kikosi cha Geita Gold FC, Fred Felix Minziro amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana kuifikisha timu hiyo hapo ilipo licha ya changamoto nyingi walizopitia msimu huu.

Geita inashikilia nafasi ya sita kwa alama 37 ikipambana kumaliza ndani ya tano bora katika michezo miwili iliyosalia kabla ya kufungwa pazia la ligi msimu wa 2022-23.

Minziro alifafanua kwamba haikuwa rahisi kwa timu hiyo kuendelea kupambana na kufika hapo ya hapo licha ya kuondokewa na wachezaji wao wengi waliokuwa wakiunda kikosi cha kwanza cha timu hiyo iliyoshiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa mara ya licha kwanza msimu huu.

“Kama ilivyoonekana wachezaji wengi waliondoka kwenye dirisha dogo la usajili na wengi walikuwa ni kikosi cha kwanza lakini wachezaji waliobaki walipambana, tukawa pamoja na tumefika hapa nawapongeza sana.

“Bado tunajipanga kuhakikisha tunamaliza ligi ndani ya tano bora, tunapishana pointi mbili na Namungo walio nafasi ya tano, hivyo bado tuna nafasi na wachezaji wapambanaji ninao pia,” amesema Minziro.

Miongoni mwa nyota walioihama timu hiyo katika dirisha dogo ni Saido Ntibazonkiza aliyeenda Simba, Yahya Mbegu aliyetua Ihefu, Kevin Nashon na Yusuf Kagoma waliotimkia Singida BS na George Mpole aliyesajiliwa FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Wakurugenzi kamilisheni miradi kwa wakati - Senyamule
Ukitaka uzuri sharti udhurike - Wahenga