Shirikisho la soka duniani FIFA limemuongezea adhabu ya kutojihusisha na shughuli za soka aliyekua rais wa chama cha soka nchini Ghana (GFA) Kwesi Nyantakyi, kwa siku 45 zaidi.

Nyantakyi aliadhibiwa kwa kosa la kupokea rushwa Juni 08 mwaka huu, na adhabu yake iliyotolewa na kamati ya maadili ya shirikisho hilo ilipaswa kuchukua muda wa siku 90.

Kwa mantiki hiyo adhabu ya Nyantakyi ambayo ilipaswa kufikia kikomo leo Septemba 06, itaendelea kwa muda wa mwezi mmoja na nusu.

Kamati ya maadili ya FIFA ilitumia ushahidi uliofanywa kwa uchunguzi wa kina, na kubaini Nyantakyi alipokea fedha taslimu kama zawadi.

Mdau huyo wa soka barani Afrika alipigwa picha za video kwa siri, zikimuonyesha akipokea burungutu la fedha (Dola za Marekani 65,000 sawa na Pauni 48,000).

Shughuli ya upigaji picha hizo za video ilifanywa na mwandishi wa Ghana Anas Aremeyaw Anas, na baadae zilitumika katika vipindi mbalimbali vya televisheni ikiwepo shirika la habari za Uingereza kupitia kipindi chake cha “Africa Eye”.

Baada ya Nyantakyi kuadhibiwa na FIFA, alitangaza kujizulu nafasi zake zote ndani ya chama cha soka nchini Ghana, CAF na FIFA.

Mdau huyo alikua mjumbe wa mkutano mkuu wa FIFA na makamu wa rais wa CAF.

Simon Mignolet aenguliwa kambi ya Ubelgiji
Majaliwa: Tanzania tumenufaika na mkutano wa FOCAC

Comments

comments