Mshambuliaji kutoka nchini Poland Robert Lewandowski amezima mbio za baadhi ya klabu za barani Ulaya ambazo zilionyesha nia ya kumsajili mwishoni mwa msimu huu, kwa kukubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu ya Bayern Munich.

Lewandowski amethibitisha kuendelea kuwepo Allianz Arena kwa kusaini mkataba wa miaka mitano ambao utamuweka klabuni hapo hadi mwaka 2021.

Mkataba wa awali wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 ulikua unamalizika mwaka 2019, na tayari mabingwa wa soka barani Ulaya pamoja na vinara wa ligi ya nchini Hispania Real Madrid, walionyesha nia ya kutaka kumsajili mwishoni mwa msimu huu.

Msimu uliopita Lewandowski aliifungia FC Bayern Munich mabao 30 katika michezo 32 aliyocheza na alitangazwa kuwa mfungaji bora wa ligi ya nchini Ujerumani.

Kwa msimu huu Lewandowski ameshafunga mabao 11 katika michezo 14 ya ligi ya nchini Ujerumani aliyocheza, na kwa upande wa ligi ya mabingwa barani Ulaya amefunga mabao matano .

Akizungumza kupitia tovuti ya FC Bayern Munich, Lewandowski ambaye ni nahodha wa timu ya taifa lake la Poland alisema: Nimefurahishwa na tukio hili la kusaini mkataba mpya, ninajivunia kuendelea kuwa hapa. Naamini kwa pamoja tutafanikisha malengo.

Naye mkurugenzi mtendaji, Karl-Heinz Rummenigge, aliongeza: “Nimefurahishwa na nimefarijika sana kuona tukio hili limefanikiwa, tunaamini kuendelea kuwa na Lewandowski ni hatua kubwa kwetu na kwa klabu kwa ujumla.”

Lowassa adai TB Joshua amemtabiria urais 2020
Arsenal Waonja Shubiri Goodison Park, AFC Bournemouth Yachanua