Beki mzaliwa wa Ufaransa Lionel Zouma, anatarajiwa kulitumikia kwa mara ya kwanza taifa lenye asili ya wazazi wake (Jamuhuri ya Afrika Ya Kati), baada ya kutajwa kwenye kikosi kitakachocheza michezo miwili ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2021) juma lijalo.

Jamuhuri Ya Afrika Ya Kati itacheza dhidi ya Burundi Novemba 13, kabla ya kuanza safari ya kuelekea mjini Nouakchott kuwakabili wenyeji wao Mauritania siku sita baadae.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 26, ni ndugu wa beki wa mabingwa wa Europa League Chelsea Kurt Zouma.

Lionel ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya ligi daraja la pili Ufaransa club Bourg-en-Bresse, ni miongoni mwa wachezaji 22, waliotajwa na kocha Francois Zahoui kuunda kikosi cha Jamuhuri Ya Afrika Ya Kati, tayari kwa michezo ya kundi E.

Hata hivyo Lionel amewahi kuitumikia timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 19 ya Ufaransa, lakini sheria za shirikisho la soka duniani FIFA zinamruhusu kubadilisha taifa, kutokana na kutopata nafasi ya kuitwa kwenye kikosi cha wakubwa cha nchi hiyo.

Aliwahi kuitwa kwenye kikosi cha Jamuhuri Ya Afrika Ya Kati kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Equatorial Guinea mwaka 2017, lakini hakufanikiwa kucheza.

Katika hatua nyingine kiungo Geoffrey Kondogbia, ambaye aliifungia klabu yake ya Valencia katika ushindi wa mabao manne kwa moja dhidi ya Lille siku ya Jumanne, amerejea kwenye kikosi cha Jamuhuri Ya Afrika Ya Kati, baada ya kushindwa kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Niger, kufuatia majeraha yaliyokua yakimkabili.

Cedric Yambere na Amos Youga wanaocheza soka la kulipwa nchini Saudi Arabia, nao wameitwa kwenye kikosi cha Jamuhuri Ya Afrika Ya Kati.

Trump atakiwa kurudisha mamilioni aliyotumia kwenye uchaguzi
Bangura asamehe yaliyotokea Sierra Leone mwezi Septemba

Comments

comments