Kocha wa Young Africans Luc Eymael amesema kuna mtu (Hajui Ni Nani) alimtumia ujumbe kumweleza kwamba David Molinga amegoma kusafiri kwenda Shinyanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mwadui FC.

Eymael amesema ameambiwa Molinga analalamika kwamba kocha msaidizi Charles Boniface Mkwasa hamkubali, Eymael amesema hawezi ku-comment chochote kwa sababu hakuwepo kwenye mazoezi yote ambayo wachezaji walifanya chini ya Mkwasa.

Kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji aliwasili nchini jana Jumatano, na leo alitarajiwa kuelekea Shinyanga na baadhi ya wachezaji kupitia Mwanza kuungana na waliosafiri jana kwa njia ya barabara.

Wakati huo huo uongozi wa Young Africans umesema kuwa upo tayari kwa ajili ya mchezo wao wa ligi dhidi ya Mwadui FC utakaopigwa Juni 13 Uwanja wa Kambarage.

Afisa Habari wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli amesema kuwa ni jambo la kusmhukuru Mungu kwa kuwa wamefika kambini salama.

“Safari yetu ilikuwa nzuri na tulifika jana kwani hapa sio mbali ukizingatia kwamba tulikuwa na usafiri wetu wa basi, ila tulipata hitilafu kidogo ambayo ilikuwa ni ajali hilo halipo juu ya uwezo wetu, hakuna anayeomba ajali.

“Licha ya ajali hiyo bado Mungu alitupigania na tumetoka salama katika hilo kwani tairi lilipata hitilafu kisha tukaendelea na safari, kwa sasa tunaanza maandalizi ya kujiweka sawa kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Mwadui tuna amini tutafanya vizuri,” amesema.

Young Africans ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na alama 51 baada ya kucheza michezo 27 ya ligi.

Magufuli: Tusidharau dawa za kienyeji "Uchawi ndiyo mbaya"
Manara: Tutafikisha alama 100 VPL, tutatwaa ubingwa ASFC