Baada ya Fernando Hierro kutangaza kujiuzulu nafasi ya ukurugenzi wa ufundi wa shirikisho la soka nchini Hispania pamoja na nafasi yake ya benchi la ufundi la timu ya taifa ya nchi hiyo, aliyekua meneja wa klabu ya Barcelona Luis Enrique ameanza kuhusishwa na mpango wa kupewa nafasi ya kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa.

Jina la Enrique limeanza kutajwa mwishoni mwa juma lililopita, huku kamati kuu ya shirikisho la soka nchini Hispania ikitarajia kukutana leo jumatatu saa tano na nusu (11:30) kwa saa za nchi hiyo, kujadili mambo mbalimbali, likiwepo hilo la kocha mpya.

Mbali na jina la Enrique kuibuka na kujadiliwa sana katika vyombo vya habari, pia majina ya makocha wengine yanatajwa katika mpango huo kama Quique Sanchez Flores, Michel, Roberto Martinez na Victor Sanchez del Amo.

Enrique kwa sasa hana mkataba na klabu yoyote, na amekuwa na uzoefu wa michezo ya kimataifa kupitia kibarua alichokitumikia akiwa FC Barcelona.

Sababu nyingine inayompa nafasi kubwa Enrique kujadiliwa sana na wadau wa soka nchini Hispania, ni kuwa na uwezo wa kuwanoa wachezaji wenye majina (Mastaa), jamba ambalo mara nyingi huwapa changamoto makocha wengi duniani.

Akiwa na FC Barcelona alifanikiwa kutwaa mataji yasiyopunguza tisa kuanzia mwaka 2014/17, huku mwaka 2015 ukiwa na mafanikio makubwa kwake baada ya kutwaa mataji matatu kwa mpigo.

Aliwahi kufanya kazi na klabu ya Celta Vigo (2013/14) na AS Roma (2011/12).

Mchakato wa kumsaka kocha mpya, unaanza kujadiliwa baada ya kufukuzwa kwa kocha Julen Lopetegui, siku mbili kabla ya kuanza fainali za kombe la dunia huko Urusi, kufuatia kutangazwa kuwa meneja wa klabu ya Real Madrid, na nafasi yake ilichukuliwa kwa muda na Fernando Hierro.

Kocha mpya atakaetangazwa na shirikisho la soka nchini Hispania, atasainishwa mkataba wa miaka miwili, na kazi kubwa itakayomkabili ni kuipeleka timu ya taifa hilo kwenye fainali za mataifa ya Ulaya mwaka 2020.

Ripoti: Wafanyakazi hulipa kodi zaidi ya waajiri
Lugola afunguka tena kuhusu watu wanaopotea

Comments

comments