Rais John Magufuli amebatilisha hati ya shamba lenye ukubwa wa hekta 33 lililokuwa likimilikiwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, lililoko eneo la Mwabepande jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya uamuzi huo wa Rais Magufuli imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi aliyeeleza kuwa Sumaye ameshindwa kuliendeleza ndani ya muda wa siku 90 alizopewa katika notisi.

“Oktoba 28 mwaka huu, Rais John Magufuli alibatilisha hati ya kumiliki ardhi ya shamba namba 3074 lililoko Mabwepande,” alisema Hapi. “Shamba hili lilikuwa na hati namba 53086, jina la mmiliki lililoandikwa katika hati ni Frankline Sumaye,” aliongeza.

Hapi alisema kuwa vyombo vya dola vitalisimamia shamba hilo ambalo hivi sasa liko chini ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni likisubiri utaratibu wa kuwauzia kwa bei nafuu wananchi waliokuwa wamelivamia.

Watu zaidi ya 100 wakiwemo waliobomolewa nyumba zao katika maeneo ya mabondeni walivamia shamba hilo mwaka jana na kujikatia maeneo.

Akizungumzia taarifa za uamuzi uliofikiwa na Rais Magufuli, Sumaye alisema kuwa hana taarifa hizo kwakuwa yuko nje ya mkoa wa Dar es Salaam.

“Unataka niseme nini wakati umeniambia Rais amebatilisha? Alihoji, “Ila niseme tu nikirudi Dar es Salaam nitalifuatilia na kuchukua hatua zinazostahiki,” mwanasiasa huyo mkongwe anakaririwa na Mwananchi.

Lowassa awafungukia wanasiasa waliodai ni ‘mgonjwa atakufa’
Video: Lyaniva azitaka taasisi za kidini kujitolea damu