Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameligeukia tena sakata la kifo cha Faru John akiiweka kando ripoti ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyowasilishwa kwake Desemba 9 mwaka huu, iliyodai faru huyo alikufa Agosti 18 mwaka huu.

Jana, Waziri Mkuu alisema kuwa ameunda timu nyingine itakayofuatilia undani wa kifo cha Faru John ikiwa ni pamoja na kulifukua kaburi lake na kufanya vipimo vya vinasaba ili kutambua kama pembe iliyowasilishwa kwake ni ya faru huyo ama la.

Majaliwa ameonesha kutoridhishwa na taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyoongozwa na Waziri mwenye dhamana, Profesa Jumanne Maghembe, akieleza kuwa haikuonesha namna ambavyo Faru huyo aliugua na jinsi alivyopata matibabu ya kidaktari kabla ya kufariki Agosti 18.

“Ili kupata ukweli na usahihi wa taarifa niliyoipata awali, ninataka Hifadhi ya Grumet kujiridhisha kama kuna kaburi la Faru John. Lakini hatuishii hapa, lazima tufuatilie na vinasaba vitakavyopatikana kwenye kaburi, ili vihusishwe na pembe niliyonayo,” Waziri Mkuu anakaririwa.

Waziri Mkuu alisema kuwa timu hiyo itahusisha vinasaba vitakavyopatikana na vinasaba vya watoto wanaodaiwa kuwa ni wa Faru John ili kujiridhisha kama kweli aliyekufa ni faru huyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kati ya watoto 37 walio katika hifadhi hiyo, 26 (sawa na asilimia 70.2 ni watoto wa Faru John.

Joshua Nassari aipongeza Serikali, aahidi ushirikiano
Mugabe achaguliwa kugombea tena urais 2018