Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa miezi mitatu kwa wananchi wote waliojenga ndani ya eneo la mpaka wa Tanzania na Zambia kubomoa nyumba zao na kuiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanza kuweka alama za X katika nyumba 252 zilizojengwa ndani ya mpaka huo ili wahusika wazibomoe.

Agizo hilo amelitoa mapema hii leo alipotembelea eneo la ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha (OSBP) katika mpaka wa Tanzania na Zambia, ambacho kinajengwa na Serikali ya Tanzania na kinatarajia kugharimu takribani sh. bilioni 12.

“Kuna watu wamejenga ndani ya mpaka wa Tanzania na Zambia na kuendesha biashara zao jambo ambalo ni kinyume cha sheria na linazikosesha Serikali mapato,Hatuna msamaha kwa watu waliojenga katika eneo hili kwa sababu wamesababisha tupoteze kodi nyingi, hivyo baada ya kumalizika muda huo mamlaka husika zibomoe nyumba zote zitakazosalia.”amesema Majaliwa.

Aidha, Kufuatia hatua hiyo Waziri Mkuu ametoa muda wa miezi mitatu kwa watu wote waliojenga kuanzia umbali wa mita 50 kutoka Tanzania na mita 50 kutoka Zambia kuzibomoa nyumba hizo kwa hiari.

Vile vile Majaliwa amekutana na Mkuu wa wilaya ya Nakonde nchini Zambia, Field Simwinga ambaye amesema kuwa wamekubaliana na utekelezaji wa agizo hilo kwa kuwa jambo hilo linaathiri shughuli za mipakani kwa pande zote mbili.

Hata hivyo, Simwinga amesema kuwa tayari wameshaanza kuwaeleza wananchi wao waliojenga ndani ya mpaka huo kuanza kuondoka, ambapo Waziri Mkuu amesema wanataka eneo hilo liwe wazi ili iwe rahisi kuutazama mpaka huo kwa umakini.

 

 

Majaliwa awataka NHC kujenga nyumba katika maeneo mengine ya utawala
Lissu achukuliwa vipimo vya mkojo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali