Je ni hatua gani umepiga katika maisha yako ?

Usijibu kwa sababu mshahara ni mdogo, au kazi imebana, hapa nataka ujipe jibu halisi, kwa nini umeshindwa kupiga hatua? Kwa sababu nina imani kuna ambao wanafanya kazi kama yako, na wanalipwa kama unavyolipwa wewe ila wao inawezekana wamepiga hatua kuliko wewe. Hivyo hapa njoo na sababu za upande wako, achana kufikiria sababu za mwajiri wako kwa muda.
Inawezekana hujaweza kujitengenezea nidhamu ya fedha, kwamba ukipata mshahara unautumia wote mpaka unaisha halafu unaanza kukopa. Na hapa mara nyingi itakuwa imeanzia kwenye kushindwa kudhibiti matumizi yako na hatimaye yanakuwa yamezidi kipato.

Inawezekana pia una wategemezi wengi wa moja kwa moja na hivyo kipato chako kugawanywa mara nyingi na kukufanya ushindwe kupiga hatua.
Na pia inawezekana una matumizi mengi yasiyo ya msingi, labda umekuwa unanunua vitu kwa kusukumwa na hisia tu. Vitu kama nguo, au kutembelea maeneo ya starehe na kadhalika.Hapo nimetoa tu maeneo ambapo matatizo yako ya fedha yanaweza kuwa yanachochewa zaidi, ila wewe ndiye unayejua kwa upande wako ukweli uko wapi.

Kwa nini ni muhimu sana kujiuliza na kujijibu swali hilo?
Ni muhimu sana ujiulize na kujipa majibu ya swali hilo la kuhusu mchango wako wewe kwenye hali yako ya kipato kuwa ngumu. Hii ni kwa sababu hata kama utaacha kazi na kwenda kwenye ujasiriamali, sio kwamba tabia zako zitabadilika pale pale. Unaweza kwenda nazo kwenye ujasiriamali na mambo yako yakazidi kuwa magumu kuliko hata yalivyokuwa mwanzo.
Ni vyema ukajua ni wapi unapochangia ili uweze kujirekebisha kabla hujaingia kwenye ujasiriamali

Video: Wito uliotolewa na Wazee Chadema kwa Rais JPM
Video: Serikali kuboresha nyumba za kurekebishia tabia watoto