Diego Maradona ameponda uteuzi wa kocha wa timu ya taifa ya Argentina Jorge Sampaoli, kwa kusema bado ugonjwa wa timu hiyo haujapatiwa dawa inayostahili.

Maradona amesema hakubaliani na uteuzi wa kocha huyo, kwa kuangalia kigezo cha kuwa muwezeshaji wa kikosi cha Chile kutwaa ubingwa wa mataifa ya kusini mwa Amerika (Copa America) mara mbili mfululizo.

Amesema pamoja na kuuponda uteuzi wa kocha huyo kutoka nchini Argentina, bado ataendelea kuwa mstari wa mbele kuungana na viongozi wa chama cha soka (AFA), kwa maamuzi ya kumfuta kazi kocha aliyetangulia Edgardo Bauza, ambaye alishinda michezo mitatu kati ya minane, iliyoshuhudia akiwa katika benchi la ufundi la timu ya taifa ya nchi hiyo.

Sampaoli mwenye umri wa miaka 57, alikabidhiwa kikosi cha Argentina mwezi Mei, na tayari amekiongoza kikosi cha nchi hiyo katika michezo miwili dhidi ya Brazil na Singapore na kufanikiwa kushinda yote.

“Sampaoli hana uwezo kumzidi Bauza, japo wote siwakubali,” Maradona aliiambia Argentine channel TyC.

“Kama Sampaoli alishindwa kuifunga Argentina wakati wa fainali za mataifa ya kusini mwa Amerika mwaka 2015 (Copa Amerika), katika mchezo wa fainali, inadhihirisha hana uwezo mkubwa wa ukufunzi wa soka, hususan kuifundisha timu yetu.”

Maradona pia amempinga Sampaoli kwa maamuzi ya kumuweka nje ya kikosi mshambuliaji wa Manchester City Sergio Aguero, wakati wa mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Brazil na Singapore.

“Ilikua sawa na ukichaa kwa maamuzi ya kumuweka nje Kun (Aguero),” Aliongeza Maradona.

“Kun ana heshima yake katika kikosi cha timu ya taifa, ana uwezo wa kukimbia, kushambulia na wakati mwingine anasaidia kuzuia mashambulizi, sasa unawezaje kumuweka nje mtu kama huyu? Aliohoji Maradona.

Mara kadhaa Maradona amekua mkosoaji na mpongezaji kuhusu timu ya taifa lake la Argentina, japo aliwahi kuwa kocha mkuu wa timu hiyo na kushindwa kufikia lengo la kutwaa ubingwa wa fainali za kombe la dunia mwaka 2010.

Sumaye aiangukia Serikali, aomba kukivumilia Chadema
Ndanda FC Waibuka Na Mbinu Mbadala