Mbunge wa Jimbo la Dokololo kutoka nchini Uganda, Cecilia Barbara amesema kuwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ni msaada mkubwa kwa Afrika Mashariki kwasababu itasaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wa moyo wanaopelekwa India au Afrika ya Kusini kwaajili ya matibabu.

Ameyasema hayo mapema hii leo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, amesema kuwa kutokana na ubora wa huduma zinazotolewa tangu kuanzishwa kwake taasisi hiyo itakuwa tegemeo kubwa kwa Afrika Mashariki.

“Tunahitaji kubadilishana mawazo kama wana Afrika Mashariki, kwa sababu kwa kuja hapa tumegundua tuna vifaa ambavyo vitasaidia kupunguza gharama za matibabu na kuleta unafuu kwa wagonjwa wa moyo,”amesema Barbara.

Amesema kuwa Serikali ya Uganda imekubali kuja Tanzania kuutembelea mradi huo ili waweze kujifunza ni namna gani shughuli za taasisi hiyo zinavyofanyika katika uendeshaji wake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Prof. Mohamed Janabi amesema kuwa wanatoa huduma kwa watu wote kuanzia daraja la chini na watu kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Uganda, comoro, Yemen na Kenya.

Hata hivyo, Prof. Janabi ameongeza kuwa kwa mgonjwa mmoja wa maradhi ya moyo anatibiwa kwa shilingi milioni 35-40 tofauti na nchini India ambapo mgonjwa mmoja anatumia shilingi milioni 120.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na Mbunge wa Ilala, Azzan Mussa Zungu (CCM) amesema kuwa wamewapeleka wageni hao kwenye taasisi ya moyo ili waweze kujifunza na kuona ni jinsi gani Tanzania imefanikiwa kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa wa moyo.

Magazeti ya Tanzania leo Julai 13, 2017
TFF Yaanika Mambo Hadharani