Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi mhandisi wa ujenzi wa wilaya ya Morogoro, Brown Undule baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ikiwemo usimamizi mbovu wa ujenzi wa kituo cha Afya Mkuyuni.

Amemsimamisha kazi Mhandisi huyo leo, baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya akiwa katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro, amesema hajaridhishwa na aina ya milango iliyotumika.

“Milango yote katika jengo hili ing’olewe leo leo, huwezi kuweka milango ya hovyo namna hii yaani mtu wa nje anamuona aliyeko ndani, nimesitisha kuendelea kukagua jengo. Yeye na usomi wake ameridhishwa na milango ya hovyo kama hii.” amesema Majaliwa

Waziri Mkuu amesema aina ya milango iliyowekwa katika kituo hicho cha afya haiwezi kutumika hata kwenye nyumba ya mtu binafsi, lakini kutokana na uangalizi mbovu kutoka kwa watendaji walikubali kuweka milango hiyo mibovu.

Amesema Serikali imeamua kujenga vituo vya afya vitano kwenye wilaya hiyo ili kusogeza huduma za afya kwa wananchi na kuwapunguzia kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, hivyo amewataka watendaji wasimamie ipasavyo miradi hiyo.

Na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuboresha huduma za afya kwa wananchi, hivyo amewataka wananchi hao waendelee kuwa na imani na Serikali yao.

Baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya, Waziri Mkuu amekagua ujenzi wa hospitali ya wilaya, ambapo ameagiza kung’olewa kwa mbao zote zilizotumika kwa ajili ya kupaulia jengo la mama na mtoto la hospitali hiyo kwa kuwa hazina viwango.

Kwa upande wake fundi anayejenga jengo hilo la mama na mtoto, Johnson Ishengoma amesema changamoto kubwa anayoipata katika ujenzi huo ni ucheleweshwaji wa vifaa pamoja na kulazimishwa kutumia vifaa vilivyo chini ya kiwango.

Fundi huyo ametolea mfano suala la mbao za kupaulia kuwa aliomba mbao za urefu wa futi 20 lakini aliletewa mbao zenye urefu wa futi 12 na kulazimishwa azitumie hivyo hivyo.

“Mhandisi wa wilaya Brown Undule na mtu wa manunuzi Grace ndio wanaoniletea vifaa hivi. Baadhi ya vifaa huwa navikataa kutokana na kutokuwa na ubora.” amesema fundi Ishengoma.

 

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Septemba 19, 2019
Profesa Kabudi amuaga Balozi wa Rwanda, aeleza walichofanikisha