Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jamii Media Limited inayoendesha mtandao wa Jamii Forums, Mexence Melo, ameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es salaam baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Melo ametimiza masharti ya dhamana baada ya kushindwa kufanya hivyo mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha kwenda gerezani.
Aidha, Melo amesema kukamatwa kwake ni ishara mbaya kwa vyombo vya habari, kwani ni shambulizi kwa uhuru wa vyombo vya habari na imekuwa ni mara ya kwanza mtu kuwekwa ndani kwa kulinda uhuru wa kuongea.
“Nawahakikishia watumiaji wa mtandao wa Jamii Forums kwamba upo salama na hakuna taarifa zozote zilizochukuliwa wala zitakazochukuliwa na mtu yeyote”amesema Melo.
Melo anakabiliwa na kesi tatu kwa mahakimu watatu tofauti, kesi namba 457 iliyokuwa kwa Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa ndiyo aliyoshindwa kutimiza masharti.