Msanii maarufu wa nyimbo za injili nchini Ghana, Brother Sammy amekamatwa kwa tuhuma za kutangaza bidhaa zake alizodai zinatibu Virusi vya Ukimwi.

Brother Sammy amekuwa akitangaza kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, akieleza kuwa maji yake aliyoyaita ‘Spiritual Divine Holy Water’ yanaweza kuponya Ukimwi.

Mwimbaji huyo ambaye jina lake halisi ni Samuel Opoku, alidai kuwa ameshawatibu watu 50 na kwamba kwa siku moja amekuwa akiuza chupa 50 za maji hayo kwa watu mbalimbali nchini humo na nchi jirani.

Hata hivyo, Mamlaka ya Vyakula na Dawa nchini humo (FDA) imeeleza kuwa bidhaa yake hiyo haijakaguliwa na haijathibitishwa kuwa na uwezo anaoutangaza.

Brother Sammy ambaye alitamba zaidi na wimbo wake wa mwaka 2017 uitwao ‘Amen’, ameachiwa kwa dhamana na anatarajia kufikishwa mahakamani hivi karibuni, kwa mujibu wa mwandishi wa BBC aliyeko Ghana.

Watu kadhaa ambao wanajitambulisha kama wataalam wa tiba za asili nchini humo wamekuwa wakijitokeza kudai wamepata dawa ya Virusi vya Ukimwi, lakini wamekuwa wakizuiliwa kutokana na kutothibitishwa.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Juni 25, 2019
Cardi B apagawa na muziki wa Afrika

Comments

comments