Mwenyekiti wa klabu ya Young Africans Dk Mshindo Msolla amesema mshambuliaji wa zamani wa klabu hiyo Amisi Tambwe atalipwa fedha zake kwa utaratibu ambao wamekuwa wakiutumia kuwalipa wote wanaoidai.

Msolla ametoa kauli hiyo ikiwa ni muendelezo wa taarifa iliyotolewa jana jioni na Uongozi wa klabu hiyo, kuhusu taarifa walioipokea kutoka FIFA, ambayo inawataka kumlipa Tambwe stahiki zake.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na kaimu katibu mkuu wa Young Africans Haji Mfikirwa, ilikanusha tetesi za klabu hiyo kufungiliwa kusajili kwa misimu mitatu, kufuatia kosa la kukaidi kumlipa mshambuliaji huyo kutoka nchini Burundi ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya Polisi nchini Djibout.

Msolla amesema young Africans imekua na utaratibu wa kulipa madeni ya wachezaji na watendaji wengine waliowahi kufanya kazi klabuni hapo, hivyo ni jambo la kusubiri na kufuatwa kwa utaratibu waliojiwekea.

“Naomba ifahamike, tuna utaratibu wetu wa kulipa madeni, tumekuwa tukilipa kidogo kidogo hata FIFA wanafahamu. Ndio utaratibu tuliotumia kuwalipa waliokuwa makocha wetu George Lwandamina na Mwinyi Zahera”

“Hivyo niseme tu Tambwe nae atalipwa kwa utaratibu huo lakini siwezi kusema ni mpaka lini tutakuwa tumemalizana nae muhimu tu ifahamike kuwa tutamlipa,” alisema

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM, Mhandisi Hersi Said amesema hadi kufikia Ijumaa (kesho) watakuwa wameilipa fedha yote wanayodaiwa na Amis Tambwe.

Hersi amesema sakata hili lilijitokeza kabla ya ujio wao lakini wanawahakikishia Wananchama na Mashabiki wa Young Africans wanakua na amani na klabu yao kwa kufanikisha mpango wa kulipa deni hilo.

Rage: Young Africans lipeni deni la Tambwe
Tanzania, Burundi kutopewa chanjo ya Corona