Kocha mkuu wa klabu ya Young Africans Zlatko Krmpotic amesema laiti kama kungekua na muda wa juma moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu msimu wa 2020/21, angetafuta mchezo mwingine wa kirafiki ili kujiridhisha utayari wa kikosi chake.

Kocha Zlatko ametoa kauli hiyo baada ya kuanza kazi ya kukiongoza kikosi chake katika mazoezi tangu mwanzoni mwa juma hili kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria kilichoko jijini Dar es Salaam akiwa na wachezaji wote waliosajiliwa akiwamo mshambuliaji mpya kutoka Burkinafaso, Yacouba Sogne, ambaye aliwasili nchini Jumatatu.

Kocha huyo amesema wachezaji wake wamefanya mazoezi vema, lakini anasikitika kukosa muda wa kucheza mchezo wa ya kirafiki ili kuwaimarisha kabla ya kuanza msimu mpya.

“Ingekuwa vema kama tungepata mchezo wa kirafiki, lakini muda ni mfupi kabla ya kuanza kwa ligi, tunaendelea na maandalizi na naamini mambo yataenda katika mstari tunaoutaka,” amesema Zlatko.

Ameongeza kama angepata muda wa wiki mbili au tatu, angepata muda wa kufanya majaribio ambayo yangewaimarisha wachezaji wake na kupata kikosi imara zaidi kitakachokuwa tayari kupambana.

“Kuna programu ya mazoezi nimeiandaa, tutaitumia kwa kipindi hiki kilichobakia ili kuweka muunganiko mzuri kwa wachezaji,” Zlatko amesema.

Young Africans wataanza Mshike Mshike wa Ligi Kuu mwishoni mwa juma hili  kwa kuwakaribisha ‘Maafande’ wa Jeshi la Magereza, Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini.

Sven: Hakuna mchezo rahisi mbele yetu
Mwinyi arejesha fomu ZEC