Ommy Dimpoz ameyajibu maswali ya mashabiki na wadau wa muziki waliokuwa wakihoji alipozipata pesa za kula bata nono katikati ya Dubai huku akiwa kimya kimuziki.

Dimpoz ambaye ameutambulisha wimbo wake mpya wa ‘Cheche’ akiwa chini ya menejimenti mpya ya ‘Rockstar4000’, amefunguka leo kwenye The Playlist ya 100.5 Times Fm kuwa maisha yake ya anasa mithiri ya bilionea katikati ya Falme za Kiarabu yaliwezeshwa na idara ya utalii ya Dubai.

Alisema wakati anaingia Dubai aliweka kwenye mtandao wake picha inayoonesha anaingia na kwamba idara hiyo ya utalii ilimtafuta kupitia hashtag aliyoiweka na kisha kumtumia barua pepe kumuomba wampe ofa ya kutalii ili aitangaze zaidi.

“Walinitafuta kupitia hashtag ya #hellowDubai ambayo niliiweka kwenye picha yangu ambayo ilipata likes zaidi ya 15,000 na comments nyingi. Nadhani walipoangalia akaunti ina katiki ka blue (imethibitishwa), wakanitafuta kwenye mitandao kuona ni nani huyu. Na unajua wakiingia google wanaona ni msanii wa Tanzania…,” Ommy alifunguka.

“Kwahiyo waliniita tukafanya makubaliano ya wapi na wapi natakiwa kufika na kufanya nini. Ilikuwa ofa kubwa sana kiasi kwamba kuna maeneo hata sikuweza kufika,” aliongeza.

Aliwataja watu wengine maarufu ambao waliwahi kupata bahati ya kupewa ofa kama hiyo kwa kuweka hashtags za #hellodubai #welcomeDubai #VisitDubai kwenye mitandao yao ya kijamii ni pamoja na bingwa wa dunia wa masumbwi ya uzito wa juu, Anthony Joshua na mwimbaji Banky W.

Magazeti ya Tanzania leo Julai 9, 2017
Fred Matiang'i ateuliwa kukaimu kiti cha waziri usalama Joseph Nkaissery