Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana alifanya ziara kwenye Bandari ya Tanga na kubaini ukiukwaji wa taratibu za manunuzi uliogharimu dola milioni 10.1, ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 21, kununua Matishali zisizohitajika.

Waziri Mkuu alibaini kuwa Bandari hiyo ilitumia kiasi hicho cha fedha kununua matishali tatu kutoka nchini China zilizo na ubora unaokinzana na mahitaji ya awali yaliyobainishwa kwenye nyaraka za maombi ya kufanya ununuzi.

Uongozi wa Bandari hiyo ulinunua Matishali tatu zinazosukumwa wakati mahitaji ya awali yaliyobainishwa yalikuwa ununuzi wa matishali mbili zinazojiendesha zenyewe.

“Kwahiyo, walileta  matishali matatu kwa bei ndogo wakati sisi tulitaka matishali mbili zinazojiendesha zenyewe. Mlidhani mtaleta nyingi ili tuone mmeleta nyingi, kumbe mmeleta vitu ambavyo hatuvihitaji,” alisema Waziri Mkuu.

Kufuatia sakata hilo, Mhandisi wa Bandari hiyo, Sifael Felix alilazimika kutoa majibu ya mchakato huo baada ya Kaimu Meneja wa Bandari hiyo, Henry Arika kumueleza Waziri Mkuu kuwa wakati ununuzi huo unafanyika hakuwa katika bandari hiyo.

Felix alikiri kuwepo kwa mabadiliko yasiyofuata utaratibu wa ununuzi na kueleza kuwa Bandari hiyo haina uwezo wa kufanya ununuzi hivyo ilipeleka mahitaji yake Makao Makuu Dar es Salaam ambao walifanya ununuzi huo unaokinzana na ‘specification’ zilizowekwa kwenye nyaraka za bandari hiyo.

“Mheshimiwa sisi hatukufanya ununuzi, tuliagiza kutoka Tanga Port kwenda makao makuu, kwahiyo Makao Makuu ndio  waliofanya procurement process, tuliagiza Matishali mawili lakini yakaletwa matatu” alisema Filex.

Baada ya maelezo ya kina, Waziri Mkuu aliagiza uongozi wa Bandari hiyo kumpa maelezo kwa maandishi ndani ya saa 16 kuanzia muda huo.

“Maelezo hayo nayataka kwenye maandishi kesho saa sita mchana (Jumamosi). Ueleze nani anayehusika kikamilifu,” aliagiza Waziri Mkuu.

Kadhalika, aliutaka uongozi wa Bandari hiyo kuhakikisha unadhibiti uingizwaji wa sukari kutoka nchini Brazil.

 

Kinachojiri Uganda baada ya Mpinzani wa Museveni kutiwa Mbaroni tena
SDL Mzunguko Wa 9 Wikiendi Hii