Sakata la mali zinazodaiwa za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda limeendelea kulitikisa bunge baada ya Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) kuongeza nyingine.
Akichangia taarifa za Kamati za Bunge za Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Selasini amesema Makonda amenunua jengo (apartment), lenye thamani ya Sh. 600 milioni.
“Makonda amenunua apartment pale Viva Towers kwa Sh. 600 milioni amempa mke wake gari aina ya Mercedes Benz lenye thamani ya Dola 250,000 za Marekani (Sh. 550 milioni) kama zawadi ya ‘Birthday’,” amesema Selasini.
Aidha, suala la utajiri wa Makonda, liliibuliwa bungeni kwa mara ya kwanza Februari 6 na Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Msukuma akitaka mteule huyo wa Rais achunguzwe kwa kujilimbikizia mali.
Vile vile Msukuma alifikia hatua hiyo ya kutaka mali za Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kuchunguzwa baada ya  hatua yake ya kutangaza majina ya watu aliodai wanajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya, huku akidai kuwa utajiri wake una shaka.
Msukuma Februari 7, mwaka huu aliomba mwongozo kwa Spika, akitaka Bunge litoe mwongozo kuhusu utajiri huo wa Makonda ndani ya muda mfupi.
Hata hivyo, mbali na mali hizo Msukuma alisema Makonda anamiliki magari mengine ya kifahari aina ya V8, anajenga maghorofa jijini Mwanza na amekarabati ofisi yake kwa Sh400 milioni bila kutumia utaratibu wa sheria ya manunuzi.

Askofu Gwajima kununua treni ya umeme
Video: Fahamu ulipofikia mradi wa barabara ya Makumbusho Jijini Dar