Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa kiasi cha shilingi bilioni 2.4 kwa ajili ya kuboresha mradi wa maji katika mji wa Makambako mkoani Njombe.

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati akizungumza na wananchi katika uwanja wa Polisi Makambako ulipofanyika mkutano wa hadhara akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Njombe.

Majaliwa asema lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata maji safi za salama katika umbali usiozidi mita 400 kama inavyosema sera ya maji.

Hivyo, amewataka wananchi kutofanya shughuli za kijamii katika vyanzo vya maji ili kuvilinda. Amesema Serikali inatumia fedha nyingi kutafuta maji kwa sababu vyanzo vingi zimekauka kutokana na shughuli za kibinadamu.

Aidha, Majaliwa amezungumzia suala la madai ya fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa kituo cha ukaguzi cha pamoja na soko la kitamaifa katika eneo la Makambako aliahidi kuwa watalipwa.

“Fidia zenu mtalipwa hivi katibuni baada ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kukamilisha taratibu za ulipaji,” amesema. Wananchi hao walilalamikia ucheleweshwaji wa malipo ya fidia hizo kupitia katika mabango mbalimbali pamoja na mbunge wa Njombe, Deo Sanga.

Serikali imeanzisha eneo la Idofi lililoko Makambako kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja wa magari ya mizigo ili kupunguza vikwazo vya kibiashara barabarani kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo kituo hicho kitakuwa na vituo vidogo vya Polisi, Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Maliasili pamoja na vituo vya mizani.

Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa jimbo la Njombe, Sanga amesema moja ya changamoto inayowakabili wakazi wa mji wa Makambako ni ucheleweshwaji wa malipo ya fidia kwa waliopisha ujenzi wa kituo hicho hali inayosababisha baadhi yao kwenda kudai fidia hiyo kwake.

”Mheshimiwa Waziri Mkuu leo na sisi wananchi wa Makambako tutapona. Baba Majaliwa hawa wananchi wanadai fidia yao kwa muda mrefu na baadhi yao wamefikia hatua ya kuja kulala nje ya nyumba yangu wakigoma kuondoka hadi niwape ufafanuzi wa malipo yao,” amesema.

Naye Mkuu wa wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amesema Serikali imetenga sh. bilioni 2.8 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la chuma lenye urefu wa mita 95 katika mto Ruhuhu.

Amesema mkataba wa ujenzi wa nguzo za daraja tayari umesainiwa kati ya mkandarasi wa kampuni ya M/s Lukolo na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa gharama ya sh bilioni 6.17 na muda wa utekelezaji ni miezi 24.

 

Video: Majaliwa aagiza elimu itolewa kwa wahudumu wa Hoteli na 'Gesti'
Liverpool Wagoma Kumuuza Mamadou Sakho