Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imejipanga kuhakikisha inaweka mkakati madhubuti na endelevu wa kuwapata wanufaika stahiki wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kuwapatia ruzuku zao kwa wakati.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa wakati akizungumza na wananchi na wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Vijiji vya Magata na Kyamyorwa, wilayani Muleba mkoani Kagera ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani humo ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa kuanzia sasa wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini watasajiliwa katika mfumo wa kielektroniki ikiwa ni pamoja na kupigwa picha kwa anayesajiliwa na anayesajili wakiwa katika makazi ya mnufaika ili kujiridhisha na sifa za mhusika.

Aidha, Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa, katika kuboresha utekelezaji wa Mpango wa TASAF awamu ya tatu sehemu ya pili, wanufaika wa Mpango watapatiwa ruzuku yao kwa njia ya miamala ya simu ili wapate stahiki zao kwa wakati.

“Wanufaika mnatakiwa kuwa na simu za viganjani zitakazowawezesha kupokea ruzuku zenu halisi na kwa wakati,”amesema Dkt. Mwanjelwa

Hata hivyo, Dkt. Mwanjelwa amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kuwajali wanyonge hivyo, itahakikisha kila mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini anapata stahiki yake.

Obama akerwa na viongozi wanaotoa kauli za kibaguzi na chuki
Video: JPM ataka SADC ya viwanda, Mwandishi ashtakiwa kwa kesi ya uhujumu uchumi