Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali tayari imeshalipa sh. bilioni 722.7 kati ya sh. bilioni 964.2 za madeni ya michango ya jumla ambayo Serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii nchini.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Oktoba 20, 2016) wakati akifungua Mkutano wa Sita wa wadau wa NSSF ulioanza leo kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Arusha na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 600.

Amesema sekta hiyo imekua kwa asilimia 15 kutoka sh. trilioni 8.9 mwaka 2015 hadi kufikia sh. trilioni 10.2 mwaka 2016. “Hadi kufikia Juni 2016, takwimu zinaonesha idadi ya wanachama imeongezeka na kufikia milioni 2.1. Rasilmali za mifuko zimefikia shilingi trilioni 10.28 na mafao yaliyolipwa kwa kipindi cha mwaka kinachoishia Juni 2016 ni shillingi trilioni 2.93. Michango ya wanachama kwa mwaka ni shilingi trilioni 2.15 uwekezaji katika nyanja mbalimbali umefikia kiasi cha shilingi trilioni 9.29,” ameongeza.

Waziri Mkuu pia amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Prof. Godius Kahyarara awaandikie barua waajiri wote wanaodaiwa na shirika hilo na kuwataka wawasilishe fedha wanayodaiwa mara moja na wale ambao hawatalipa ndani muda utakaowekwa wafikishwe mahakamani na yeye apewe taarifa.

“Kumekuwepo na changamoto ya muda mrefu ya baadhi ya waajiri kutolipa michango kwa wakati hali inayoleta usumbufu mkubwa kwa wanachama hasa wanapofikia muda wa kustaafu. Suala hili halikubaliki, hivyo natoa maelekezo kwa waajiri wote nchini waheshimu sheria na wawasilishe michango yao kwa wakati,” amesisitiza.

Mbali ya kuwabana waajiri, Waziri Mkuu pia amewataka wanunuzi wa nyumba za shirika hilo na wapangaji wote wanaodaiwa wakamilishe malipo yao na wasipofanya hivyo ndani ya muda uliopangwa wafikishwe mahakamani.

“Nimeambiwa pia lipo tatizo la wadaiwa wa nyumba yaani wanunuzi na wapangaji. Suala hili lilitolewa maelekezo na Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu. Nataka nisisitize kuwa watu wote walionunua nyumba za NSSF na bado hawajakamilisha malipo na wale waliopanga lakini hawalipi kodi wanatakiwa kulipa haraka au wakabidhi nyumba hizo kwa NSSF ziuzwe kwa watu wengine, vinginevyo nao wafikishwe mahakamani.”

Akizungumzia utendaji wa shirika hilo, Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wa shirika hilo na Bodi ya Wadhamini kwa uamuzi wake wa kuwekeza kwenye uzalishaji wa sukari nchini. Amesema kiwanda kitakachojengwa, kinatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 100,000 kwa Watanzania na hivyo kuongeza wanachama katika mfuko wa NSSF.

“Nimefurahishwa na uamuzi wa NSSF na PPF kuungana ili kukabiliana na tatizo la sukari nchini. Tumeelezwa hapa kuwa mashirika haya yatashirikiana kujenga Kiwanda cha Sukari kitakachozalisha tani 200,000 kwa mwaka. Kiwanda hicho kitajengwa katika eneo la Mkulazi lililopo mkoani Morogoro,” amesema.

Akiwasilisha msaada huo, Prof. Wangwe alisema wameguswa na tatizo lilitokea mkoani Kagera na wameamua kutoa mchango ili kusaidia juhudi za Serikali kukabiliana na maafa hayo. Pia alisema wamekamilisha ahadi yao ya madawati 6,000 yenye thamani ya sh. milioni 400 ambayo waliitoa awali.

 

TASWA Kuongoza Kongamano La Mabadiliko Simba, Yanga
Wanafunzi UDSM wagoma, wapinga punguzo la kiwango cha mkopo