Serikali imezindua mpango kazi wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto unaolenga kushirikisha wadau wengine katika jitihada jumuishi za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto hivyo kusaidia wahanga wa ukatili huo kupata huduma stahiki ili kudhibiti ukatili nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kwa niaba ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa jamii inajukumu la kuhakikisha ukatili wa wanawake na watoto unapigwa vita kwa vitendo.

“Serikali inaikumbusha jamii kupambana na vitendo vya ukatili kwani ukatili unafanyika kuanzia ngazi ya familia hivyo ni jukumu la wananchi kutoa taarifa za ukatili wa wanawake na watoto ili vyombo vya dola viweze kuwachukulia hatua za kisheria”, amesema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Asasi za Kiraia zinazoshughulika na utetezi wa haki za watoto (TCRF)  Erick Guga amesema kuwa watoto ndiyo wahanga wakubwa wa ukatili huu hivyo ni wakati muafaka kwa mpango kazi kuanza kazi ili kuwanusuru wanawake na watoto katika ukatili.

Mpango huu mahususi unatarajiwa kuwa na matokeo makubwa baada ya miaka mitano ya utekelezaji kwani utawezesha kuondoa ukatili dhidi ya wanawake kwa asilimia 50 kufikia mwaka 2021/2022; na Kuondoa ukatili dhidi ya watoto kwa asilimia 50 kufikia mwaka  2021/2022, na hivyo kuleta mabadiliko makubwa kwa kuwa na familia salama, na jamii yenye utulivu.

Kazi zitakazotekelezwa na kila mdau kuanzia familia, jamii, halmashauri, mikoa, wizara, sekta binafsi, asasi za Kiraia na wabia wa maendeleo Mpango umeweka mfumo fungamanishi wa uratibu, ufuatiliaji na tathmini ambao utaratibiwa katika ngazi ya Taifa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ngazi ya mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, na ngazi ya halmashauri na Wakurugenzi Watendaji.

Makonda azindua ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita moja jijini Dar
Video: Magufuli afanya mabadiliko makubwa CCM