Rapa Nikki wa Pili aliwahi kughani, ‘hakuna aijuaye kesho hata mtunzi wa kalenda’. Hii imedhihirishwa pia na Snoop Dogg ambaye amewashangaza wengi kwa kutangaza kuachia albam ya nyimbo za injili. Ndio… ni Snoop huyu aliye miongoni mwa majina ya ‘gangsta rappers’.

Akifanya mahojiano na kituo cha redio cha Beats One, rapa huyo mwenye umri wa miaka 45, amefunguka kuwa kwa muda mrefu amekuwa akisikia msukumo moyoni mwake kuwa anapaswa kufanya muziki wa injili na kwamba anaona sasa ndio muda muafaka.

“Ninatayarisha albamu yangu ya muziki wa injili,” alisema Snoop. “Imekuwa moyoni mwangu kila wakati. Sikuwahi tu kupata muda wa kuishughulikia kwa sababu tulikuwa tunafanya biashara za ‘kigenge’ au kufanya vile. Nimefikiria tu kwamba imekuwa ndani ya moyo wangu kwa muda mrefu. Nahitaji kuifanya…. Nafanya sasa,” alifunguka.

VIDEO: Magari matano yenye kasi #ZAIDI duniani (S01E01)

Aliongeza kuwa ana mpango wa kuwashirikisha mastaa wengine kwenye albam hiyo akiwemo Faith Evans, Charlie Wilson na Jeffery Osborne.

Hii sio mara ya kwanza kwa rapa huyo nguli kubadili muelekeo wa muziki wake. Miaka ya hivi karibuni alifanya albam yenye mahadhi ya reggae aliyoipa jina la ‘Reincarnated’, aliyodai kuwa imetokana na kuingiwa na mzuka wa Bob Marley. Snoop alibadili pia jina kutoka kuwa Snoop Dogg na kuwa Snoop Lion.

Stamina amnyooshea mikono Dk. Mwakyembe, ‘nimebadilika'
?Live: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Mei 22, 2017