Rais wa Marekani, Donald Trump ameonesha kuchukizwa zaidi na jaribio kubwa la makombora ya nyuklia lililofanywa hivi karibuni na Korea Kaskazini na amelitaja taifa hilo kama ‘sikio la  kufa lisilosikia dawa’, kuwa halielewi.

Trump ametumia mtandao wa Twitter kulaani vikali majaribio hayo aliyoyataja kama vitisho vya makombora ya nyuklia dhidi ya Marekani.

“Maneno yao na vitendo vyao vimeendelea kuwa hatari sana kwa Marekani,”  ametweet Trump.

“Korea Kusini inajaribu, kama nilivyowaeleza kuwa majadiliano yao na Korea Kaskazini hayatazaa matunda, Korea Kaskazini wataelewa kwa kitu kimoja tu,” aliongeza.

Ingawa hakuweka wazi kitu anachoamini kitawafanya waelewe, Trump amewahi kusema kuwa ataishambulia Korea Kaskazini kama itaendelea na majaribio ya makombora ya nyuklia na vitisho dhidi ya Marekani.

Amesema China ambayo ni mshirika mkubwa wa Korea Kaskazini haioneshi ushirikiano unaoridhisha kumaliza mgogoro huo kidiplomasia.

Marekani ilipendekeza vikwazo zaidi vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini lakini nchi hiyo imeendelea kupuuza hatua za vikwazo hivyo.

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong -Un alisema nchi yake haiogopi vikwazo na kwamba itajibu kwa vita kamili kama itaguswa kwa shambulio lolote.

Urusi imeendelea kuikingia kifua Korea Kaskazini ikieleza kuwa mazungumzo ndio njia pekee ya kuutatua mgogoro huo.

 

 

 

Magazeti ya Tanzania leo Septemba 4, 2017
Baada ya 2Pac Chid Benz ampa shavu Jay z