Baada ya kuitumikia timu ya taifa ya Nigeria kwa kipindi cha miaka sita, mshambuliaji wa pembeni Victor Moses, ametangaza kustaafu soka la kimataifa akiwa na umri wa miaka 27.

Mshambuliaji huyo ambaye wakati mwingine hutumika kama beki wa pembani akiwa na klabu ya Chelsea, ametangaza maamuzi hayo huku akiwa amecheza michezo 37 kwenye kikosi cha Nigeria.

Mara ya mwisho alionekana na timu hiyo wakati wa fainali za kombe la dunia nchini Urusi, ambapo Nigeria ilitolewa hatua ya makundi, ikitanguliwana Croatia, Argentina na Iceland ilishika mkia wa kundi.

“Nimepata ujuzi wa kutosha, nimejifunza mambo mengi nikiwa na timu ya taifa langu, sina budi kutangaza kustaafu kucheza soka la kimataifa kuanzia leo, nitabaki kuwa shabiki na mtazamaji,” Ameandika Moses katika ukurasa wake wa mtandao wa kjamii wa Twitter.

“Ninaamini muda huu ni muafaka kwangu kuchukua maamuzi haya, ninatarajia kuona vijana wakipewa nafasi kubwa katika timu ya taifa ya Nigeria ili kuwezesha malengo yanayokususdiwa na viongozi wa chama cha soka NFF na mashabiki.”

Moses alikuwa sehemu ya kikosi cha Nigeria kilichotwaa ubingwa wa Afrika mwaka 2013, na kuisaidia nchi hiyo kutinga katika hatua ya 16 bora ya michuano ya kombe la dunia, mwaka 2014.

Kwa upande wa klabu amewahi kutwaa ubingwa wa England akiwa na klabu ya Chelsea msimu wa 2016-17, lakini kwa msimu huu bado hajapata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza chini ya utawala wa meneja mpya Maurizio Sarri.

NEC yaujibu ubalozi wa Marekani, yautaka utoe uthibitisho
Serengeti Boys uwanjani leo