Serikali kupita Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limefanya ukaguzi wa miradi mikubwa 163 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 2 ikijumuisha Barabara, majengo, maji na viwanja vya ndege.

Hayo yamesemwa mapema hii leo na Kaimu wa Idara ya Uhandisi wa Baraza hilo, Mhandisi Wambura M Wambura alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya ukaguzi huo.

Wambura amesema kuwa miradi  yote iliyofanyiwa ukaguzi inatekelezwa chini ya ufadhili wa Serikali.

“Shughuli za kiukaguzi zilizofanyika ni pamoja na kufanya mapitio na tathmini ya michakato ya manunuzi, utekelezaji wa mikataba, utekelezaji wa miradi,ongezeko la gharama za miradi, pamoja na ubora wa kazi zilizofanyika,” amesema Wambura.

Aidha,Wambura amesema kuwa katika kipindi cha 2015/2016 baraza lilifanya ukaguzi wa kiufundi wa miradi ya matengenezo ya barabara kwa halmashauri zote za Wilaya pamoja na TANROADS kwa Mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, na Shinyanga ambapo miradi hiyo iliyotekelezwa kwa fedha za mfuko wa Barabara.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Idara ya majengo, Kissamo Elias ametoa wito kwa wadau wa sekta hiyo kulitumia Baraza hilo kufanya kaguzi katika miradi wanayotekeleza ili kuongeza tija hali itakayochochea ukuaji wa sekta hiyo.

Baraza la Taifa la Ujenzi ni kitovu cha uratibu wa sekta ya ujenzi kwa taasisi zote zinazoshughulika na shughuli za ujenzi pamoja na wadau ili kuleta umoja,uwiano, na ushirikiano katika utendaji ndani ya sekta ya ujenzi,Baraza linaendelea kusimamia na kuongoza juhudi za kukuza na kuendeleza sekta ya ujenzi nchini.

 

Video: Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki kutembelea Tanzania
Live Washington: Sherehe za kuapishwa Donald Trump kuwa Rais Marekani