Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema kuwa watu wanaodai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli ni ‘Dikteta’ hawajui maana ya kile wanachokizungumza.

Nchemba amesema kuwa watu hao aliodai wanalalamika na kulialia kuhusu utawala wa sasa ni wale wasiofuata sheria kwani Serikali ya awamu ya Tano inaongozwa kwa kufuata sheria.

“Niwaambie tu kwamba kama hawawajui madikteta waende upya wafuatilie dikteta anakuaje, nikwambie hata kwa maeneo ambayo tumewahi kuona yakiwa na viashiria vya kidikteta kwanza mtu kusema tu huyu ni dikteta kwanza anakuwa ashakimbia kwenye hiyo nchi,” Nchema anakaririwa.

Aliwashangaa watu hao wanaozungumzia kuwepo kwa udikteta nchini wakati wanaendelea na shughuli zao za kawaida, wanaenda kwenye starehe na ratiba za kila siku bila kusikia hukumu yoyote ikitolewa moja kwa moja na Rais bali vyombo vilivyopewa jukumu hilo kisheria.

Aidha, Waziri Nchemba aliwataka kujikumbusha kuhusu madikteta waliowahi kutokea ambao walikuwa wanatoa hukumu moja kwa moja na kufikia hatua ya kuwanyonga watu hadharani.

“Kuna watu waliwahi kunyongwa uwanja wa taifa na anayesimamia zoezi hilo ni kiongozi yeye mwenyewe yaani hawajapitia hatua hata ya mahakama, yeye mwenyewe kiongozi ndiye anaamuru wanyongwe,” alisema.

Alisisitiza kuwa Rais Magufuli anachofanya ni kuwasimamia wanyonge na kuhakikisha watu wanaishi kwa kufuata sheria za nchi, na kila maamuzi yanayotolewa yanafuata utaratibu wa kisheria bila kujali matabaka ya kipato.

Serikali Yashauliwa Kusimamia Miradi Ili Kuhakikisha Malengo Yanafikiwa
Ongeza thamani yako