Uongozi wa klabu ya Young Africans umesisitiza msimu huu una jambo lao na kwamba hawana muda wa kubembeleza mchezaji, kama akipigiwa simu halafu asipokee au akikosa mchezo ajue namba inachukuliwa na wengine.

Hayo yamewekwa wazi na mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Young Africans, Eng. Hersi Said ambapo amesema hawana nafasi ya kumbembeleza mchezaji kama atashindwa kufuata matakwa na miongozo ya timu kwa sasa kikosini.

Amesema jambo hilo limeanza kuonekana kwenye kikosi chao, huku akitolea mfano wa Kiungo kutoka DR Congo Mukoko Tonombe ambaye alikosa michezo minne ya Ligi Kuu msimu huu.

Tonombe alionekana kwa mara ya kwanza kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ambao ulimalizika kwa Young Africans kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, huku kiungo huyo akipachika bao la tatu.

“Nyie si mmeona kuna mchezaji juzijuzi alifunga bao akamwaga machozi, si mmeona wenyewe. Hakuna anayetaka kupoteza nafasi yake kikosini,” amesema Hersi.

“Young Afruicans inalipa mishahara yenyewe. Ina mifumo yake ya kuajiri watu sisi tunasapoti tu. Young Africans ni timu kubwa huwezi kufananisha na wengine.”

Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 15 baada ya kucheza michezo mitano, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 11 na Polis Tanzania inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 10 sawa na Dodoma Jiji FC.

Senzo ajitosa sakata la GSM kushambuliwa mitandaoni
Mama Mzazi wa Marehemu Hamza afariki Dunia.