Kikosi cha Young Africans rasmi kimeingia kambini tayari kwa maandalizi ya mchezo wa mzunguuko wasita wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC.

Young Africans itakua mgeni katika mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Ilulu mjini Lindi, huku wenyeji wao Namungo FC wakiwa katika mazingira magumu baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Simba SC.

Young Africans waliweka kambi ya siku saba visiwani Zanzibar kwa wachezaji ambao hawakuitwa kwenye vikosi vya timu ya taifa na kucheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Mlandege na KMKM, ikiwa ni maandalizi ya michezo iliyopo mbele yao.

Kocha Mkuu wa klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Nasreddine Nabi amesema kambi ilianza rasmi jana Jumatatu (Novemba 15), kwa ajili ya kujiwinda na mchezo dhidi ya Namungo FC.

“Tulikuwa na wakati mzuri Zanzibar, tumepata nafasi ya kupanga mambo yetu, licha ya ushindi tuliopata visiwani humo katika michezo yetu miwili, lakini kuna mambo mengi tumeweza kuyaboresha pamoja na kuwa na wachezaji wachache.

“Hatuna michezo iliyokuwa rahisi kwetu, tumewaona Namungo FC wanavyocheza tumeanza kufanyia kazi mapungufu yetu na ubora wa Namungo FC, kuhakikisha tunaendelea kupata matokeo chanya na kufikia malengo yanayotarajiwa ya kutwaa ubingwa,” amesema Nabi.

Nyota wa Young Africans ambao waliitwa kwenye vikosi vya timu za taifa ni Khalid Aucho (Uganda), kipa Djigui Diarra (Mali), Ramadhan Kabwili, Kibwana Shomari, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Zawadi Mauya, Feisal Salum (wote Tanzania) na Djuma Shaban (DR Congo).

Kumwembe: Mashabiki wa soka kuweni na heshima
Tammy Abraham: Mourinho amenibadilisha