Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma limemtaka Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kuwasilisha vielelezo vya madai yake kuwa yametokea mauaji eneo la Nguruka wilayani Uvinza mkoani humo na watu 100 kupoteza maisha.

Jumapili iliyopita Oktoba 28,2018, Zitto alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kudai kuwa takribani siku 10 zilizopita yalitokea mauaji hayo na taarifa alizonazo ni kuwa watu zaidi ya 100, wakiwamo polisi walikufa.

Jana Jumanne, Oktoba 30, 2018, Kamanda wa polisi mkoani Kigoma, Martin Ottieno alizungumza na waandishi wa habari na kusema tuhuma alizotoa Zitto hazina ukweli wowote. Alisema hakuna watu 100 waliouawa na kusisitiza kuwa ni upotoshaji unaofanywa na wanasiasa.

“Hakuna watu mia moja waliouawa. Tunamtaka Zitto aonyeshe vielelezo vya hayo anayosema au aje atuonyeshe makaburi ya watu hao anaosema wameuawa Kigoma, ” alisema Ottieno.

Kamanda huyo amewataka wanasiasa kuchukua tahadhali kwa taarifa wanazopewa na watu mbalimbali kabla ya kuzisambaza ili kuepuka kupotosha jamii.

Rais Trump apigwa marufuku kutumia wimbo wa 'Happy'
Nesi akiri kuua wagonjwa 100