Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere huwa anakumbukwa kwa mambo mengi mazuri aliyoiachia nchi yake ya Tanzania na Afrika kwa ujumla, ikiwemo umoja, mshikamano na amani.

Katika mambo ambayo hayatasahaulika kumuhusu Hayati rais Nyerere ni  pamoja na kusisitiza kuwa mtu akiwa Kiongozi basi anatakiwa awe na kitu cha ziada na ndiyo maana Mwalimu alikuwa anasema mtu akiwa Kiongozi ni sharti ajiheshimu, kama uhuni basi akaufanyie barabarani na pia akasisitiza juu ya kutatua matatizo ya Wananchi.

Moja ya nukuu zake katika hili aliwahi kusema kuwa, “hatuwezi kuwa na matumaini ya kutatua matatizo yetu kwa kujifanya kuwa hayapo,” akimaanisha ni lazima kufikiria juu ya changamoto tulizonazo badala ya kuyafunika kwa kudhani yameisha.

Mwalimu alituasa sana kuwa unapokuwa Kiongozi hakikisha pia unajenga tabia ya kujisomea, ili kila uchwao upate maarifa na taarifa mpya ikiwezekana kabla ya Watu unaowaongoza.

Aidha, aliasa kila siku kuwa Kiongozi lazima apime kila anachotaka kuzungumza kwa umma maana maneno ya Kiongozi siku zote ni nukuu na ndiyo maana tunaona mpaka leo, watu wengi bado wananukuu Maneno ya Mwalimu Nyerere.

Siku hizi Kiongozi akiongea na umma, badala ya kufundisha, kuonesha njia, kuwa mfariji na hata kuwaweka Watu pamoja, yeye anageuka kuwa mfitini, kinara wa kukashifu, kinara wa Propaganda nk.

Waweza isikiliza hotuba ya Kiongozi kuanzia mwanzo mpaka mwisho ukasikia anashambulia watu, anasifia watu, anatumia maneno ambayo hata mtu ambaye siyo Kiongozi anabaki na maswali kama anayezungumz ni Kiongozi kweli?

Hapo lazima utajiuliza je, hiki anachozungumza kinaweza tumika kama nukuu kwa vizazi vijavyo? ni kwanini baadhi ya Viongozi hawachagui maneno, hawafundishi, hawaunganishi watu, haheshimu Katiba, Sheria, Kanuni, taratibu na tamaduni zetu?

Hata hivyo ni yeye pia Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, “itakuwa yote ni makosa na si jambo la muhimu kuhisi kuwa lazima tusubiri hadi viongozi wafe ndio tuanze kuwakosoa.”

Wahenga walipata kusema ‘Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’ lakini pia wakaongeza ‘Samaki mkunje angali mbichi’ haitoshi wakaongeza tena jingine ‘mdharau mwiba mguu huota tende’ wakatoa na nyongeza kwamba ‘usipoziba ufa utajenga ukuta,’ bula shaka sauti imesikika.

Benchikha atoa ya moyoni Mapinduzi CUP
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Januari 15, 2024