Kiungo Mshambuliaji ‘Winga’ wa Tanzania Simon Msuva, amesema ubora aliokuwa nao katika michuano ya Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’, ni moja ya sababu za yeye kusaini katika klabu ya A-Najma inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini Saudi Arabia.

Akifanya mahojiano nchini Ivory Coast, Msuva amesema baada ya kuachana na JS Kabylie ya Algeria, alipata ofa nyingi lakini aliamua kuichagua Al-Najma.

“Kwa kiasi kikubwa ‘AFCON 2023’ imenisaidia kulikuza zaidi jina langu, baada ya funga bao katika mchezo wa pili dhidi ya Zambia, niliendelea kupata ofa nyingi zaidi nashukuru Mungu kwa hili,” amesema.

Amesema sasa ataonekana katika ligi ya Saudi Arabia na anafurahi kuitumikia klabu yake hiyo kwa msimu mwingine baada ya kumaliza majukumu ya timu ya Taifa.

“Nafurahi kupata timu na kuerejea katika ligi ya Saudi Arabia, huko ndiyo nitakapoonekana kwa sasa, kuna ofa nyingi zilikuja ndani na nje ya Tanzania, Al-Najma walikuwa na ofa nzuri,” amesema.

Amesema alikuwa ana ofa nchi za Uturuki, China na lraq alichagua Saud Arabia kwa sababu anajua faida zake, aliwahi kucheza nchini humo hivyo hakujiuliza mara mbili baada ya ofa hiyo.

“Mimi ndiyo najua nini nataka katika maisha haya, najua kuna watu watashangaa kwa nini nimeenda kucheza ligi daraja la pili, kikubwa nawaahidi Watanzania nitapambana kuhakikisha naiwakilisha vyema Tanzania,” amesema.

Al-Najma ni timu ya tano kwa nyota huyo nje nchi tangu alivyoondoka Young Africans msimu wa 2017/18, amepita Difaa El Jadida na Wydad Casablanca za Morocco, Al Qadsiah ya Saudi Arabia na JS Kabylie ya Algeria ambayo ametoka hivi karibuni.

Vitisho sababu Chamisa kujiuzulu CCC
Wavuvi haravu wakumbushwa nguvu ya Dola