Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko leo amefanya ukaguzi wa mitambo ya umeme inayokarabatiwa katika kituo cha umeme cha New Pangani (MW 68) ambacho kilisimama kuzalisha umeme kwa zaidi ya wiki mbili kutokana na hitilafu na kuwaagiza Wataalam waTANESCO kufanya kazi hiyo kwa kasi na umakini ili kukamilisha matengenezo hayo ambayo yapo ukingoni.

Katika ziara yake kwenye kituo hicho kilichopo wilayani Korogwe mkoani Tanga, Dkt. Biteko aliambatana na viongozi mbalimbali akiwepo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

Amesema, “nawapongeza kwa hatua mliyofikia sasa kwenye matengenezo, lakini ni muhimu sana kuongeza kasi na umakini katika kumalizia kazi kwani Watanzania wanatutegemea sisi ili kupata umeme wa uhakika na kuelekeza kuwa, matengenezo ya kituo hicho yapo ukingoni na inategemewa kuwa wiki ijayo kitaanza tena kuzalisha umeme na hivyo kuimarisha hali ya upatikanaji umeme hasa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha.”

Aidha, ameongeza kuwa, jitihada nyingine zinazofanyika ili kuimarisha hali ya umeme kwenye mikoa hiyo ni kupitia laini ya msongo wa kV 400 itakayotoka Chalinze- Segera hadi Tanga Mjini na laini ya kV 400 kutoka Singida – Manyara- Lemuguru ambayo itaunganishwa na laini ya kutoka Chalinze kwenda Segera hadi Tanga Mjini.

Vilevile, Dkt. Biteko amewataka watendaji wa TANESCO kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye vituo vya umeme, ili kutambua mapema hitilafu za umeme na kuzifanyia kazi, huku akiwasha umeme katika Kijiji cha Ngomeni kata ya Ngomeni wilayani Muheza na kufanya vijiji vilivyowashiwa umeme wilayani humo kufikia 127 kati ya Vijiji 135 sawa na asilimia 95.

Fedha iliyotengwa kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini wilayani Muheza ni shilingi Bilioni 18.96 ambayo ni kwa ajili ya kusambaza umeme kwenye nyumba, migodi midogo, vituo vya afya, maeneo ya kilimo na pampu na za maji huku mkandarasi akiwa ni kampuni ya Derm Group.

Wageni waridhishwa hali ya usalama Arusha
Ushirikiano chanzo utekelezaji miradi ya maendeleo