Mchambuzi wa Sky Sports, Jamie Carragher anaamini klabu ya Liverpool ina nafasi kubwa ya kutwaa Ubingwa wa England msimu huu 2023/24, licha ya kufuatwa kwa ukaribu na Arsenal pamoja na Man City.

Kikosi hicho cha Kocha Jurgen Kopp kwa sasa kinashika usukani wa Ligi Kuu England, lakini Manchester City na Arsenal zipo karibu sana, sare moja tu kwa Liverpool wenzake wakishinda, wanamshusha.

Pointi mbili tu zimetofautisha timu hizo tatu na mechi bado 11 kwa kila timu.

Hata hivyo, Carragher anaamini Liverpool itapambana na kushinda taji hilo la ligi msimu huu.

Akizungumza Sky Sports, beki huyo wa zamani wa Liverpool alisema: “Nadhani tangu zilipoanza kutumika sub tano, hakuna mtu aliyeonyesha ubora mkubwa kwenye hilo zaidi ya Jurgen Klopp.

Tuliwazungumzia hapa Arsenal na sasa unafikiria wanaweza kuchukua ubingwa. Wapo vizuri sana kwenye beki na Man City wao ni bora na vipaji vya mchezaji mmoja mmoja navyo ni vikubwa, lakini Liverpool itashinda ubingwa kupitia benchi lao, kwa sababu Klopp anatumia sub tano.”

Carragher alifichua kuwa Liverpool imetumia sub 119 tangu mwanzoni mwa msimu huu, ikiwa ni idadi kubwa sana ukilinganisha na Man City iliyotumia sub 74.

Liverpool imelazimika kutanua kikosi chake kwa siku za karibuni kutokana na kuandamwa na majeruhi wengi.

Mlinda Lango Alisson anasumbuliwa na maumivu ya misuli, wakati Diogo Jota, Curtis Jones, Trent Alexander-Arnold na Mohamed Salah walikosa mechi kadhaa za mwezi uliopita.

Kwenye mchezo wa Kombe la FA, Kocha Klopp alitumia makinda ikiwamo Jaydan Danns, Jarrell Quansah, James MeConnell na Bobby Clark.

 

Siku ya Wanawake Duniani: NSSF yakabidhi Vifaa tiba Mahuta
Vita ya usajili 2024/25 imeanza